Ronaldo awa kinara ligi ya pesa 2020

Wednesday June 3 2020

 

LONDON, ENGLAND. SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amempiku staa mwenzake, Lionel Messi kwenye mchakato wa wanasoka waliovuna pesa nyingi zaidi kwa mwaka 2020 kama inavyofichua orodha mpya ya jarida la Forbes.

Mjumuiko wa mishahara yake pamoja na pesa nyingine anavuna kupitia soka lake la uwanjani pamoja na dili za matangazo umemshuhudia Ronaldo akiweka kibindoni Pauni 85.8 milioni kwa mwaka 2020, akiwa amezidiwa na staa wa tenisi, Roger Federer, ambaye anashika usukani kwa kuwa mwanamichezo aliyevuna pesa nyingi zaidi duniani.

Messi anashika namba tatu kwenye orodha yote, lakini ni namba mbili kwa wanasoka, kutokana na kuvuna Pauni 83.4 milioni, huku hilo likija baada ya Barcelona kuamua kump-unguzia mshahara wake kutokana na janga la corona.

Anayefuatia kwenye orodha ni Mbrazili, Neymar ambaye amevuna Pauni 76.6 milioni, huku staa huyo wa Paris Saint-Germain, akivuna Pauni 20 milioni kutoka kwenye dili zake za matangazo.

Staa wa Liverpool, Mohamed Salah anafuatia kwenye orodha hiyo, lakini akishika namba moja kwa upande wa Ligi Kuu England baada ya kuvuna Pauni 28.2 milioni ndani ya mwaka huu na kumpiku straika namba moja wa Ufaransa, Kylian Mbappe. Mbappe amevuna Pauni 27.1 milioni ndani ya mwaka huu, huku orodha hiyo ikiwahusu pia mastaa Andres Iniesta, anayekipiga Vissel Kobe ya Japan, kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil, staa wa Manchester United, Paul Pogba, kiungo wa Shanghai SIPG, Oscar na mkali wa Barcelona, Antoine Griezmann.


Advertisement

Advertisement