Ronaldo atabaki kuwa juu

Muktasari:

  • Ronaldo alifunga mabao mawili kwa kichwa na jingine kwa penalti na kwa kufanya hivyo ameendelea kuwa mfalme wa hatua ya mtoano katika historia ya michuano hiyo akiwa amefunga mabao 63 mpaka sasa.

TURIN ,ITALIA. KUNA kama Cristiano Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya? Hakuna. Rekodi zake zinajieleza. Na juzi Jumanne ameendelea kushindilia rekodi zake akiwaacha mashabiki midomo wazi.

Ronaldo Februari 5 mwaka huu alitimiza miaka 34, lakini ndio kwanza kama ameanza. Juzi aliwapiga Atletico Madrid Hat trick na kuipeleka Juventus hatua ya robo fainali licha ya kuchapwa mabao 2-0 katika pambano la awali jijini Madrid.

Ronaldo alifunga mabao mawili kwa kichwa na jingine kwa penalti na kwa kufanya hivyo ameendelea kuwa mfalme wa hatua ya mtoano katika historia ya michuano hiyo akiwa amefunga mabao 63 mpaka sasa.

Hasimu wake, Lionel Messi ambaye jana Jumatano na Barcelona yake walitazamiwa kuikaribisha Lyon Nou Camp anashika nafasi ya pili akiwa amefunga mabao 40 katika hatua hiyo. Raul Gonzalez anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao 34 katika hatua hiyo wakati Thomas Muller, Thierry Henry na Andriy Shevchenko wanafuatia wakiwa wamefunga mabao 21 kila mmoja.

Kwa kupiga Hat trick ya juzi, Ronaldo pia alikuwa amemfikia hasimu wake Lionel Messi katika ufalme wa wachezaji waliofunga hat trick nyingi zaidi katika michuano hiyo. Juzi ilikuwa ni hat trick yake ya nane akiwa amemfikia Messi ambaye mpaka kufikia jana kabla ya pambano dhidi ya Lyon alikuwa na idadi hiyo ya Hat trick.

Ronaldo na Messi wamewaacha mbali mastaa wanaofuatia kwa idadi kubwa ya Hat trick ambao ni Filippo Inzaghi, Mario Gomez na Luiz Adriano ambao kila mmoja ana hat trick tatu katika michuano hiyo maarufu barani Ulaya. Na sasa Atletico inakuwa timu ya pili kwa kufungwa mabao mengi na Ronaldo katika historia ya soka. Kwa mabao yake matatu ya juzi, Ronaldo anakuwa ameifunga Atletico mabao 25 huku timu ambayo ameifunga zaidi ikiwa ni Sevilla ambayo ameifunga mabao 27.

Ronaldo pia ameifunga Atletico mabao ya ugenini 10 huku akiwa amezifunga Sevilla na Barcelona mabao 12 kila moja ugenini. Ronaldo ameifunga Atletico mabao mengi zaidi ya penalti kuliko timu nyingine yoyote ile huku akiwa ameifunga penalti zote tisa alizopiga katika jezi za Real Madrid na kisha Juventus.

Ronaldo aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 80 milioni kutoka Real Madrid katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto mara baada ya kumalizika kwa pambano la juzi alitamba mabao anayofunga ndio sababu kubwa iliyopelekea Juventus imnunue.

“Ndio maana Juventus walinileta hapa, kwa ajili ya kuwasaidia vitu ambavyo hawajawahi kufanya awali. Hii ndio akili ambayo inaweza kukusaidia kutwaa ubingwa wa Ulaya. Mimi nafanya kazi yangu na nina furaha sana leo. ulikuwa usiku wa maajabu. Siku zote Atletico ni timu ngumu kupambana nayo lakini mara zote tupo imara na tumethibitisha hilo,” alisema Ronaldo.

“Tulihitaji usiku maalumu na ndivyo ilivyokuwa, sio tu kwa mabao yangu bali kwa timu nzima. Huu ndio moyo wa kucheza katika Ligi ya mabingwa. Tunajivunia sana hilo,” aliongeza staa huyo wa zamani wa Manchester United. Katika pambano hilo, kamera zilimuonyesha mpenzi wa Ronaldo, Georgina Rodriguez akilia jukwaani akiwa pamoja na mtoto wa kwanza wa Ronaldo Cristiano Junior, ambaye anakipiga katika timu ya watoto ya Juventus.