Ronaldo anaitaka tena Ballon d'Or

Muktasari:

Luka Modric alivunja utawala wa muda mrefu wa Lionel Messi na Ronaldo katika kubeba tuzo hiyo, kutokana na kiwango chake akiwa na Real Madrid na timu yake ya taifa ya Croatia na kuwa mtu wa kwanza nje ya wababe hao wawili kubeba tuzo hiyo tangu 2008.

TURIN, ITALIA.ALIPOKAMILISHA uhamisho wake wa kwenda Juventus, wengi walijiuliza ni kitu gani kingeweza kumfanya Cristiano Ronaldo adumishe ari yake ya kucheza soka la kiwango cha juu.
Lakini ‘mnyama’ huyo ametua kibabe pale Juve, amezoea mazingira na tayari amerudi tena katika kuwania tuzo ya Ballon d'Or.
Luka Modric alivunja utawala wa muda mrefu wa Lionel Messi na Ronaldo katika kubeba tuzo hiyo, kutokana na kiwango chake akiwa na Real Madrid na timu yake ya taifa ya Croatia na kuwa mtu wa kwanza nje ya wababe hao wawili kubeba tuzo hiyo tangu 2008.
Lakini akiwa na umri wa miaka 34, Ronaldo ameendelea kutisha mjini Turin, licha ya kipigo kutoka kwa Ajax katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwaharibia.
Aliongeza taji jingine la ligi msimu uliopita akibeba Scudetto na Juve na wakabeba pia ndoo ya Supercoppa Italiana, huku yeye mwenyewe akishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Italia.
Alipumzishwa katika mechi za awali za UEFA Nations League lakini akaitwa kwenye nusu-fainali dhidi ya Uswisi na kama kawa ‘mnyama’ akapiga ‘hat-trick’ na kuwapeleka Ureno fainali ambako pia akawasaidia kushinda ubingwa huo kwenye ardhi ya nyumbani dhidi ya Uholanzi.
Licha ya kwamba Virgil van Dijk wa Liverpool anapewa nafasi kubwa kutwaa Ballon d’Or mwaka huu akikabwa koo na Sadio Mane na Lionel Messi, Ronaldo amerejea anaitaka tuzo hiyo kwa mara ya sita.
"Siyo kwamba naing’ang’ania tuzo ya Ballon d’Or,” amesema Ronaldo. “Namba zangu hazidanganyi, mwaka huu nimeshinda makombe matatu na nimetisha katika Nations League pia. Nifanye nini cha zaidi labda?"