Ronaldo akiondoka Juventus haya yatakuwa maficho yake

Muktasari:

Umri wa Ronaldo umekwenda, miaka 35 kwa sasa, hivyo wanadhani haitakuwa shida sana kwao kama wataamua kumwondoa kwenye gharama zao za mishahara ya kila wiki. Hata hivyo, Juventus watahitaji ada y Pauni 62.5 milioni tu kwenye mauzo ya staa huyo.

TURIN ,ITALIA .CRISTIANO Ronaldo anaweza kupigwa chini huko Juventus baada ya mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na janga la virusi vya corona.

Supastaa huyo mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or anaripotiwa kulipwa Pauni 510,000 kwa wiki kutokana na huduma yake anayotoa kwenye kikosi hicho cha Juventus na mkataba wake unatajwa kwamba utafika mwisho 2022.

Lakini, taarifa za kutoka Italia zinadai klabu za Serie A zimeathirika sana kiuchumi kutokana na janga la corona na wanachofikiria ni kuondoa wachezaji ambao wanalipwa mishahara mikubwa kwenye vikosi ili kupunguza bili za mishahara.

Umri wa Ronaldo umekwenda, miaka 35 kwa sasa, hivyo wanadhani haitakuwa shida sana kwao kama wataamua kumwondoa kwenye gharama zao za mishahara ya kila wiki. Hata hivyo, Juventus watahitaji ada y Pauni 62.5 milioni tu kwenye mauzo ya staa huyo.

Kama Ronaldo ataaondoka Juventus, basi hizi hapa klabu tano zenye uwezo wa kunasa huduma ya Mreno huyo.

Man United

Kwa miaka mingi sana, mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakitamani supastaa wao wa zamani, Ronaldo arejee kwenye kikosi chao kupafanya Old Trafford kuwa mahali pa kutisha. Kama Juventus wanashindwa kumudu mshahara wa Mreno huyo bila ya shaka Man United wanaweza kuingia sokoni kusaka huduma kama itakuwa inapatikana ili aende akamalizie soka lake kwenye timu ambayo mashabiki wamekuwa wakimkubali kuliko kawaida. Man United waliimuuza Ronaldo kwenda Real Madrid.

Real Madrid

Hakuna ubishi Real Madrid bado inateseka kuliziba pengo la Ronaldo. Alipoondoka kwenda kujiunga na Juventus kwa ada ya Pauni 88 milioni amewaacha Real Madrid kwenye wakati mgumu wa kuziba pengo lake. Hivyo, kama ataamua kurudi Los Blancos litakuwa jambo bora litakalofurahiwa na mastaa mbalimbali kwenye kikosi hicho, huku mwenyewe akiripotiwa kutamani kurejea Santiago Bernabeu.

Inter Miami

Bosi wa timu hiyo, David Beckham bado anafukuzia wachezaji wenye majira makubwa kwenda kukifanya kikosi chake kuwa moto na Ronaldo anaweza kuwa mmoja wao. Ronaldo alirithi jezi namba 7 ya Beckham huko Man United mwaka 2003 na sasa akiwa mmiliki wa timu kwenye Ligi Kuu Marekani, anaweza kufungua milango ya kunasa huduma ya mreno huyo akakipiga kwenye kikosi chake. Bila shaka wazo la Ronaldo kwenda kucheza Marekani anaweza kulipokea kwa mikono miwili.

Paris Saint-Germain

Kutokana na Edinson Cavani kuachana na Pari Saint-Germain kwa uhamisho wa bure mwisho wa msimu huu baada ya kugomea mkataba mpya, bila ya shaka mabingwa hao wa Ufaransa watafungua milango kwa ajili ya kunasa straika mpya wa kutua Parc des Princes. Mambo yatakuwa magumu zaidi kama Neymar ataamua kurudi zake Hispania, hapo PSG itahitaji straika wa ngumu na matajiri wa kikosi hicho wanaweza kufikiria mpango wa kunasa saini ya Ronaldo.

Shanghai Shenhua

Ni kitu chenye ugumu, lakini klabu hiyo ya Ligi Kuu China bila ya shaka itahitaji mshambuliaji mpya wa kwenda kuchukua mikoba ya Odion Ighalo. Fowadi huyo Mnigeria, Ighalo amepewa ofa ya Pauni 400,000 kwa wiki abaki kwenye timu hiyo, lakini anaonekana kuwa na mpango wa kujiunga moja kwa Manchester United baada ya kufanya vizuri muda wake wa mkopo kwenye kikosi hicho. Hivyo, kama Ighalo atabaki Man United, Ronaldo anaweza kunaswa akaongoze mashambulizi.