Ronaldo afikisha mabao 700

Muktasari:

Nahodha wa Ureno Cristiano Ronaldo amefikisha mabao 700 katika mechi 976 alizocheza katika mashindano yote.

Lisbon, Ureno. Cristiano Ronaldo amefikisha mabao 700 katika mashindano yote baada ya jana kuisaidia Ureno kupata ushindi dhidi ya Ukraine.

Mshambuliaji huyo wa Juventus, amefikisha idadi hiyo baada ya kucheza mechi 976.

Nahodha huyo wa Ureno alifikisha mabao 699 katika mchezo dhidi ya Luxembourg uliochezwa Ijumaa iliyopita ambao Ureno ilishinda mabao 3-0.

Nguli huyo alifunga bao dakika ya 72 kwa penalti na kuchangia ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Ureno ikiwa ugenini katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.

Mchezaji huyo bora mara tano wa dunia,  alicheza kwa kiwango bora katika mechi zote mbili ambazo alikuwa nahodha.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, ameingia katika orodha ya wachezaji nguli waliofunga mabao 700 au zaidi kabla ya kustaafu.

Ronaldo amefikia mafanikio ya akina Josef Bica, Romario, Pele, Ferenc Puskas na Gerd Muller waliotamba kwa kufunga mabao enzi zao.

Nguli huyo amefunga mabao matano akiwa Sporting Lisbon, Man United (118), Real Madrid (450), Juventus (32) na 95 kwa Ureno.