Ronaldinho kushuhudia mechi ya maveterani Nairobi leo

Muktasari:

Ronaldinho Gaucho, aliwahi kutamba na klabu ya PSG, Barcelona na AC Milan, akitwaa mataji kibao ikiwemo ligi a mabingwa Ulaya akiwa Barcelona. Ni mshindi wa kombe la Dunia (2002), mchezaji bora wa Dunia (2004) na mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or (2005). Gaucho aliwasili nchini Kenya siku ya Ijumaa, kwa ziara ya siku tatu inayotamatika leo.

Nairobi, Kenya. Nyota wa zamani wa timu ya taifa Brazil na klabu ya Barcelona, Kiungo matata Ronaldinho Gaucho yupo nchini kwa ziara maalum ya kimichezo kwa lengo la kukuza soka la mashinani.
Gaucho ambaye ni mshindi wa kombe la Dunia (2002), mchezaji bora wa Dunia (2004) na mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or (2005), aliwasili nchini siku ya Ijumaa, kwa udhamini mnono wa kampuni ya michezo ya Extreme Sports, kwa kushirikiana na kampuni ya kubeti ya Betika.
Mara baada ya kuwasili, Gaucho ambaye anatajwa kama mmoja wa wanasoka bora kabisa ambao ulimwengu wa soka umepata kuwaona, jana Jumamosi alikuwa katika uwanja wa Camp Toyoyo kushuhudia mechi ya fainali ya makala ya mwaka huu ya ligi ya Super 8, kati ya TUK na Jericho All Stars, kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Baaada ya hapo, jana jioni alielekea mjini Kisumu, kushuhudia programu maalum ya michezo iliyofanyika ugani Moi Kisumu, kwa mwaliko maalum wa Gavana wa Kisumu, Prof. Anyang Nyong’o kabla ya kukwea pipa kurejea Nairobi.
Leo Jumapili, Novemba 11, Gaucho nyota huyo wa zamani wa PSG, Barcelona na AC Milan, anatarajiwa kumalizia ziara yake ya siku tatu nchini, atakuwa sehemu ya kikosi cha maveterani (wanasoka wa zamani) watakaokipiga dhidi ya Sofapaka inayoshiriki ligi kuu ya Kenya.
Mtanange huo maalum wa heshima, utapigwa katika uwanja wa KCB Sports, ulioko Ruaraka hapa Jijini Nairobi. Baadhi ya mastaa watakaounda kikosi hicho ni pamoja na nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Musa Otieno na Straika matata Dennis Oliech pamoja na ‘Kenya One’, Mahmoud Abbas.
Kikosi cha Malejendari wa Kenya: Mathew Ottamax, Josiah Ougo, Tom Juma, Simeone na Titus Mulama, Ramadhan Balala, Francis Oduor, Allan Wanga, Maurice Sunguti, Edward Karanja, Dennis Oliech, Victor Onyango, Mahmoud Abbas, Austin Oduor, Musa Otieno, Henry Motego.
Kocha: Jacob Ghost Mulee