Ronaldinho amkataa Messi kimtindo

BARCELONA, HISPANIA. SUPASTAA wa zamani wa Barcelona, Ronaldinho amesema tena kwa msisitizo hawezi kumchukua Lionel Messi kuwa mchezaji bora wa muda wote kuwahi kutokea kwenye mchezo wa soka.
Na badala yake, fundi huyo wa mpira kutoka Brazil, Ronaldinho alisema Messi anapaswa tu kufurahia kwa kuambiwa kuwa ni mchezaji bora katika wakati wake.
Baada ya kumshuhudia Messi akibeba tuzo ya sita ya Ballon d'Or, Ronaldinho alisema: "Nimefurahishwa na Messi kwa sababu ni rafiki yangu na zaidi ya hilo amekuwa kama bango la Barcelona.
"Sipendi sana kulinganisha kwa sababu ni ngumu kumpata mtu bora zaidi katika historia ya mchezo wa soka, kuna watu kama Diego Maradona, Pele, Ronaldo, hapo siwezi kusema Messi ni bora zaidi yao.
"Messi ni bora katika zama zake, bora katika wakati wake."
Ronaldinho alicheza soka la mafanikio makubwa akiwa na Barcelona na hata Brazil, ambapo alikuwa kwenye kikosi kilichobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2002 huko Japan na Korea Kusini huku akiwahi pia kunyakua tuzo ya Ballon d'Or.