Ronaldinho: Paraguay? Sijui kama nitarudi

Muktasari:

Na kwa mujibu wa rafiki mmoja wa karibu na Ronaldinho, Fernando Lugo, aliyemtembelea mahabusu karibuni na kupiga naye picha, amedai Gaucho ameumizwa sana na jinsi mambo yanavyoenda.

ASUNCION, PARAGUAY . RONALDINHO amesikitika na kukureka sana, lakini tabasamu lake liko palepale na ameapa msala huu ukiisha kamwe hatarudi tena Paraguay.

Gwiji huyu wa Brazil ameendelea kusota rumande karibu mwezi sasa akituhumiwa kuingia Paraguay kwa kutumia hati feki ya kusafiria ya taifa hilo la Amerika Kusini.

Na kwa mujibu wa rafiki mmoja wa karibu na Ronaldinho, Fernando Lugo, aliyemtembelea mahabusu karibuni na kupiga naye picha, amedai Gaucho ameumizwa sana na jinsi mambo yanavyoenda.

Lugo alisema; “Kuna rafiki yangu yuko rumande na aliniambia kuwa Ronaldinho anataka kuniona. Ana huzuni, lakini uso wake bado una tabasamu.

“Nadhani ana hasira na ameniambia, ‘Nchi yako kwa nini inanifanyia hivi? Kamwe sitarudi Paraguay’.”

Akizungumzia maisha ya kila siku ya Ronaldinho rumande, Lugo alisema; “Hana shida yoyote, watu wanamjali na anakula asado (chakula cha Paraguay chenye nyama na samaki) kila siku, na anakipenda sana.

“Si kwamba kila siku anajifungia kwenye selo yake tu, anapiga stori na wenzake na hukaa muda mwingi nje akishiriki michezo.”

Lugo alienda mbali zaidi na kumtetea Ronaldinho kwa kudai hana hatia na kinachofanyika sasa ni kumuonea; “Anachofanyiwa si haki. Kwa nini afanye kosa kama lile? Hana shida yoyote ya kutenda kosa lile.”

Kauli hiyo ya Lugo aliitoa wakati akielezea tuhuma kwamba staa huyo wa zamani wa Barcelona alishiriki kwenye utakatishaji pesa. Ronaldinho alienda Paraguay kushiriki kwenye tukio la kijamii lililojulikana kwa jina la Angelical Fraternity, lakini alikamatwa na polisi pamoja na kaka yake Roberto de Assis kwa tuhuma za kutumia hati feki za kusafiria mapema mwezi huu. Mshindi huyo wa zamani wa Tuzo ya Ballon d’Or, aliomba kupata kifungo cha nje wakati akisubiri hukumu yake, lakini jaji wa kesi hiyo, Clara Ruiz aligoma na kusisitiza anaweza kutoroka au kuingilia upelelezi.

Utetezi wa Ronaldinho umesimama kwenye hoja kuwa hakuwa anajua kama alipewa hati ya kusafiria iliyochakachuliwa, alihisi ni hati ya kusafiria ya heshima. Upelelezi bado unaendelea