Rodri : Jembe jipya lililovunja rekodi ya uhamisho City

Muktasari:

Ni nani huyu Rodri ambaye amesababisha Manchester City ivunje rekodi ya uhamisho ya wachezaji kwa sababu yake?

MANCHESTER, ENGLAND.HATIMAYE Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amefanikiwa kumnasa kiungo mahiri wa Atletico Madrid na Timu ya Taifa ya Hispania, Rodri.

Kiungo huyu anaonekana mbadala wa muda mrefu wa staa wa kimataifa wa Brazil, Fernandinho ambaye siku zake za kucheza soka katika kiwango cha juu zinaelekea ukingoni.

Ni nani huyu Rodri ambaye amesababisha Manchester City ivunje rekodi ya uhamisho ya wachezaji kwa sababu yake?

Atosa na Atletico atua Villarreal

Jina lake kamili ni Rodrigo Hernández Cascante lakini jina lake la kwanza linafupishwa kwa kifupi cha Rodri. Alizaliwa Juni 23, 1996 katika Mji Mkuu wa Hispania Madrid.

Kutokana na kuzaliwa Madrid, Rodri alijiunga na Shule ya Soka ya Atletico Madrid mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 11 akitokea katika timu ndogo ya mtaani ya CR Rayo Majahonda.

Hata hivyo, klabu ya Atletico ilimuacha mwaka 2013 kwa kile ilichodai kwamba hakuwa na nguvu.

Baada ya kuachwa na Atletico kwa sababu hiyo, hatimaye Rodri alinaswa na Klabu ya Villarreal ambayo iliamua kumwamini. Februari 7, 2015 akiwa bado na timu ya vijana, Rodri alicheza mechi ya kwanza katika kikosi cha wachezaji wa akiba.

Katika pambano hilo aliingia uwanjani katika dakika za mwisho dhidi ya RCD Espanyol B katika pambano la Ligi Daraja la Kwanza ambalo walishinda mabao 3-1 wakicheza ugenini. Hata hivyo, siku 15 baadae alianza mechi yake ya kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Real Zaragoza.

Mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa ilikuja Desemba 17, 2015 akianza katika ushindi wa mabao 2- dhidi ya SD Huesca pambano la michuano ya Kombe la Mfalme. Mechi yake ya kwanza La Liga ilikuja Aprili 17, 2016 katika kichapo cha mabao 1-2 ugenini dhidi ya Rayo Vallecano akiingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Denis Suarez.

Desemba 4, 217 baada ya kufanikiwa kutamba katika kikosi cha kwanza mkataba wake uliongezwa kufikia mwaka 2022. Alifunga bao lake la kwanza katika soka la kiwango cha juu Februari 18, 2018 huku timu yake ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya RCD Espanyol ugenini.

Atlético Madrid yarudi yamnasa

Mei 24, 2018 Rodri alirudi katika klabu yake ya utotoni Atletico Madrid baada ya klabu hiyo kufikia makubaliano na Villarreal kuhusu ada yake ya uhamisho. Alisaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ya Madrid ambako alizaliwa huku Atletico ikiilipa Villarreal dau la Euro 20 milioni na pamoja na ongezeko la Euro 5 milioni kutokana na kiwango chake kitakavyokuwa siku za usoni.

Rodri alijikuta akiaminiwa moja kwa moja na Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone huku kiwango chake kikilinganishwa zaidi na kiungo wa Barcelona, Sergio Busquet katika eneo la kiungo wa ulinzi ingawa Rodi alionekana kuwa mkakamavu zaidi.

Katika kikosi cha Atletico, Rodri alionekana kuchezewa rafu nyingi zaidi kuliko wachezaji wengine wa kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira lakini pia uwezo wake huo akiwa na mpira ulimfanya awe mmoja kati ya wachezaji chipukizi ambao walikuwa na mvuto zaidi uwanjani.

Kuanzia hapo Kocha wa City, Pep Guardiola alionekana kukoshwa na kiwango cha staa huyo huku kwa muda mrefu zaidi akimfukuzia ambapo inaonekana alikuwa na lengo la kumpa jukumu ambalo aliwahi kumpa Sergio Busquets katika kikosi cha Barcelona enzi hizo akiwa kocha.

Avunja rekodi City

Julai 3, 2019, Manchester City ilikubali kiasi cha Pauni 65 milioni kwa ajili ya kumnasa Rodri kutoka Atletico Madrid. Dau hilo lilikuwa katika kipengele cha mauzo cha staa huyo kwa mujibu wa mkataba wake na Atletico Madrid.

Alisaini mkataba wa miaka mitano na kwa dau hilo Rodi alivunja rekodi ya uhamisho ya Manchester City ambayo kwa mara ya mwisho ililipa dau kubwa kwa winga wa kimataifa wa Algeria, Riyad Mahrez ambaye walimnunua kwa dau la pauni 60 milioni kutoka Leicester City katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana.

Rodri anaonekana kuwa mbadala wa muda mrefu wa kiungo wa kimataifa wa Brazil, Fernandiho ambaye Mei mwaka huu alitimiza umri wa miaka 34 na uwezekano wa kucheza soka katika kiwango cha juu unaelekea ukingoni.

Atinga timu ya taifa Hispania

Rodri ameichezea Hispania katika ngazi zote za soka la vijana akianzia katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 16 kisha 19 na 21. Miaka minne iliyopita alikuwa katika kikosi cha michuano ya Euro chini ya umri wa miaka 20.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha Hispania Machi 2018 kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ujerumani na Argentina. Alicheza mechi yake ya kwanza siku tano baadaye katika pambano dhidi ya Ujerumani akiingia kuchukua nafasi ya Thiago Alcântara huku pambano hilo likimalizika kwa sare ya 1-1 jijini Düsseldorf Ujerumani.