Robben afurahia kufanya kazi na Pep, adai hakuna anayemfikia ubora

Muktasari:

  • “Alinidokeza naweza kuwa beki mzuri wa kati na akaniambia anatarajia nitafanya bidii kuelewa falsafa zake, katika falsafa za soka kwa Pep, nafasi za kiungo wa kati na beki wa kati majukumu yake yanafanana, ni kwamba unapokuwa mbele ya mabeki wa kati unakuwa kama beki mwingine wa tatu wa kati hasa tunaporudisha mpira nyuma kuanza moja.

KATIKA toleo lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi, Marti Perarnau alifanya mahojiano na mchezaji Javi Martinez kuhusu nafasi yake katika kikosi cha Bayern na namna ambavyo Pep anapenda acheze nafasi ya beki wa kati. Sasa endelea…

“Alinidokeza naweza kuwa beki mzuri wa kati na akaniambia anatarajia nitafanya bidii kuelewa falsafa zake, katika falsafa za soka kwa Pep, nafasi za kiungo wa kati na beki wa kati majukumu yake yanafanana, ni kwamba unapokuwa mbele ya mabeki wa kati unakuwa kama beki mwingine wa tatu wa kati hasa tunaporudisha mpira nyuma kuanza moja.

“Napenda kucheza nafasi ya beki wa kati kwa sababu nafikiri nafasi hiyo nikicheza nafasi hiyo nakuwa katika moja ya nafasi zilizo katika ubora wangu na umakini wa juu, ni moja ya sifa zangu muhimu na unajiona mwenye mamlaka unapokuwa katika nafasi hiyo.

Perarnau: Pep amefanya mabadiliko mengi tangu ajiunge na Bayern.

Martinez: ndio, tumekuwa kwenye mchakato wa kujifunza unaohusisha staili ya uchezaji mimi na wachezaji wengine pamoja na majukumu yanayotuhusu katika timu, mabadiliko yote yamekuwa na maana na jambo kubwa ni kwamba bado hatujafika katika ubora wa juu.

“Bado tuna kazi ya kufanya kufikia katika ubora, Pep anafanya kazi kila siku kuwasaidia wachezaji wawe katika ubora wakati wakiwa katika mapambano uwanjani.

Perarnau: Mmeshashinda mataji matatu hadi sasa lakini baada ya hapo mkaangukia pua katika ligi ya mabingwa, je ni kwa sababu timu imejiona ishafanikiwa na kuridhika baada ya mafanikio hayo?

Martinez: Hapo sasa kilichobaki ni jukumu letu kufanya bidii kusukuma mambo na kuendelea kuwa na hasira ya mafanikio, sisi ni kundi la vijana ambao tunataka kuweka alama yetu katika historia ya soka na tunatakiwa kukumbuka mambo yote ni ya wakati tulionao na si yaliyopita.

“Tunahitaji kuwa vile vile wenye hasira za mafanikio kwa wakati wote, Bayern inahitaji kuendelea kupambana kusaka mataji mapya, mara tu tutakapoanza kujifikiri sisi tuko vizuri, hapo ndipo tutakapoanza kuacha kupata ushindi.

Baada ya mazungumzo hayo na Javi Martinez, Perarnau alimgeukia Arjen Robben ambaye katika mechi ya kesho (dhidi ya Dortmund) atacheza nafasi ya mshambuliaji wa kati. Uzoefu wa Robben umekuwa tofauti na kile anachopitia Javi, Robben yeye hakuwahi kucheza mechi nyingi msimu uliopita.

Kuumia mara kwa mara kilikuwa kikwazo chake kikubwa alipokuwa katika timu za Real Madrid, Chelsea, PSV Eindhoven na hadi sasa akiwa na Bayern, lakini yote hayo kwa sasa ameyapa kisogo na katika msimu huu (2013/14) amecheza akiwa mchezaji wa kwenye kikosi cha kwanza katika mechi 37.

Kwa jumla amecheza mechi 45 msimu wote na kati ya hizo, amefunga mabao 21 na kutoa pasi 14 zilizozaa mabao, ni rekodi inayovutia kwa mchezaji profesheno wa kiwango chake.

Robben anakubaliana na rekodi hiyo, “Ingawa hata mwaka wangu wa kwanza hapa (2009/10) na mwaka uliopita (2011/12) tulioshinda mataji matatu makubwa pia ilikuwa ni miaka mizuri, kufanya kazi na Pep limekuwa jambo zuri kwa sababu amesaidia kuwa bora zaidi kwa mengi.”

“Kila kitu kimekwenda vizuri kuhusu suala la kuwa fiti, sikuwa mwenye kuumiaumia mara kwa mara tangu Januari 2013 na hilo limenisaidia kuwa katika ubora wa kiuchezaji kwa kipindi kirefu bila kushuka kiwango.

“Hata hivyo, hapana shaka jambo zuri zaidi limekuwa ni kufanya kazi na Pep, napenda dira yake katika soka hasa namna anavyofikiria.

Perarnau: Nini hasa kimebadilika katika suala zima la ujikinga na kuumia mara kwa mara.

Robben: “Ukiangalia huko nilikotoka unaweza kuona jinsi mambo yalivyoanza kuwa mazuri mara baada ya kuwa hapa na mambo yameendelea kwenda katika namna ya kimaendeleo, nimekuwa na daktari maalumu wa viungo wa kunitibu mara kwa mara ambaye hakika alikuwa akinisaidia katika mwaka wangu wa mwisho nikiwa Real Madrid na bado niko naye.

“Nafikiri katika miaka yangu mitano na Bayern Munich nimepata majeraha makubwa mara mbili tu, majeraha mengine ni madogo madogo ya kawaida, kwa kawaida wachezaji huwa na majeraha madogo wakiwa wadogo wanaibukia lakini kwangu imekuwa kinyume chake, uzoefu na ukomavu vimenisaidia sana, nazidi kuwa bora zaidi na zaidi katika kujilinda na majeraha na najisikia vizuri kwa hilo.

Itaendelea Jumamosi ijayo…