Rio na Owen wafunguka Solskjaer kupewa onyo

Muktasari:

  • Na sasa mastaa wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, Owen Hargreaves na Paul Ince wamedai kichapo hicho cha United kimekuja kama tahadhari kwa kocha wa muda wa United, Solskjaer ambaye tangu atue klabuni hapo amekuwa mbabe kwa timu pinzani.

MANCHESTER, ENGLAND.NI onyo tu. OLE Gunnar Solskjaer juzi Jumanne usiku alipewa kipigo cha kwanza tangu awe kocha wa muda wa Manchester United na tayari wakuda fulani wamemwambia kwamba hilo lilikuwa onyo tu katika safari yake.

PSG iliichapa Manchester United mabao 2-0 katika dimba lao la Old Trafford mechi ya kwanza hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa wa Ulaya (UCL) wakifunga mabao kupitia kwa beki, Presnel Kimpembe na mshambuliaji wao mahiri, Kylian Mbappe.

Ushindi huo ulikuja bila ya PSG kuwa na mastaa wao wawili mahiri, Neymar na Edinson Cavani ambao wote waliumia katika mechi za Ligi Kuu ya Ufaransa hivi karibuni na kocha, Thomas Tuchel alilazimika kukipangua kikosi chake katika pambano hilo na bado walishinda.

Na sasa mastaa wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, Owen Hargreaves na Paul Ince wamedai kichapo hicho cha United kimekuja kama tahadhari kwa kocha wa muda wa United, Solskjaer ambaye tangu atue klabuni hapo amekuwa mbabe kwa timu pinzani.

“Nadhani ni onyo kwake na hii timu ya Manchester United, lakini sidhani kama ni kitu kibaya. Nadhani ni kitu ambacho watajifunza na kuanzia sasa tutaona watajibu vipi mapigo. Nadhani katika kipindi chake United kipigo hiki ni sehemu tu ya jinsi ambavyo anaweza kujiandaa kujibu mapigo,” alisema Rio.

“Tulijua kwamba kuna wakati atafungwa, amekuwa katika mwendo mdundo wa kushangaza. Ameiamsha upya timu na ameifanya ijiamini. Hata hivyo leo (juzi) yalikuwa maji mazito na tumeona tofauti kati ya Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu,” alisema Rio.

Ferdinand aliudhika kutoona nguvu ya mashambulizi ya Unted ambayo wamekuwa wakioonyesha tangu Solskjaer alipoingia madarakani kiasi cha kudhiadhibu klabu mbalimbali nyumbani na ugenini.

“Leo sikuona ile nguvu ya kushambulia kabisa. Tumeona nguvu yao sana katika hii timu wiki chache zilizopita leo hatuona mfano wowote wa nguvu hizo. PSG ilicheza bila ya mastaa wao wawili bora wa ushambuliaji lakini walifanikiwa kuimaliza mechi na si ajabu wamemaliza hata mechi ya marudiano,” alimalizia Rio

Naye Owen Hargreaves, ambaye alikuwa pamoja na Rio kwenye studio alikisifu kiwango cha PSG huku akidai kwamba kipigo cha United kilikuwa angalizo kwa United mpya inayojengwa chini ya Solskjaer.

“Walifunga mabao mawili mazuri ya ugenini, tulisema kabla ya mechi kwamba Tuchel ni shujaa na tuliona hilo. Kilikuwa kiwango kizuri sana. Katika safu ya ulinzi, Marquinhos alikuwa mchezaji bora uwanjani na Buffon (kipa) hakuokoa hata mchomo mmoja wa hatari. Nadhani PSG ilishinda bila ya wasiwasi . Ni onyo kwa United. Wamekuwa bora mpaka sasa lakini mechi hii imeonyesha kwamba bado wana hatua nyingi,” alisema staa huyo wa zamani wa England.

Ilikuwa kitu kama hicho alichosema pia kiungo mwingine wa zamani wa Manchester United, Paul Ince ambaye awali alishasema Solskjaer amekuwa na muda mwepesi wa kuwa kocha wa United kwa sababu wachezaji wana morali lakini binafsi angempa kazi kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino.

“Matokeo ni wazi kama vile yamewapendelea Manchester United ukiangalia nafasi ambazo PSG ilikuwa nazo. Mambo yalikuwa magumu kwao. Nadhani leo wamefundishwa jinsi ya kucheza soka,” alisema kiungo huyo mtata.

Ilikuwa siku mbaya kwa United ambapo kiungo wao, Paul Pogba alipewa kadi nyekundu katika dakika za mwisho na hivyo atalikosa pambano la marudiano Machi 6.

Kuna uwezekano mkubwa Edinson Cavani akarejea katika pambano hilo lakini Neymar ataendelea kuwa nje ya uwanja na kuukosa tena mchozo huo.