Rio aijia juu Manchester United

Muktasari:

MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amesema kitendo cha timu hiyo kutosajili katika dirisha hili ni miongoni mwa mambo ambayo yanawafanya mashabiki kuwa katika sintofahamu juu ya hatma ya klabu katika msimu huu akilinganisha na klabu nyingine.

MANCHESTER, ENGLAND

MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amesema kitendo cha timu hiyo kutosajili katika dirisha hili ni miongoni mwa mambo ambayo yanawafanya mashabiki kuwa katika sintofahamu juu ya hatma ya klabu katika msimu huu akilinganisha na klabu nyingine.

United imefanikiwa kumsajili Donny van de Beek tu, kutoka Ajax kwa ada ya Pauni 40 milioni jambo ambalo linawafanya mashabiki wengi kuwa katika sintofahamu kwa kuangalia madili mengine yaliyokwama pamoja na lile la Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.

Huku wapinzani wake wakionekana kusainisha wachezaji wengi na wenye ubora bila shida yoyote huku Chelsea ikitumia jumla ya Pauni 200 milioni kwenye dirisha hili ambapo imewanyakuwa, Kai Havertz kutoka Bayer Leverkusen na Timo Werner wa RB Leipzig ambao walionekana kuuzwa kwa bei chee lakini ilishindwa kuwapata.

Ferdinand anaamini kocha wa Chelsea, Frank Lampard atafanya vizuri msimu huu kwa kuwa amesajili wachezaji ambao wameonesha kiwango kikubwa katika msimu uliopita na anaamini United ilitakiwa kufanya hivyo haraka.

Ferdinand alimtaja Sancho kama mfano wa kile kinachoendelea pale United katika soko la usajili ambaye alishindwa kusajiliwa kutokana na United kushindwa kufikia tarehe husika ya usajili ndani ya mwezi Agosti ambapo Dortmund iliiweka kama ndio mwisho wa kumuuza.

“Sancho alikuwa anazungumzwa sana katika miezi iliyopita, lakini hakuna kilichofanyika, sisemi kuwa madili haya ni rahisi kukamilika lakini tujipange.”