Ridhiwani ataka uchaguzi Yanga ili waibane Simba

Muktasari:

Ridhiwani Yanga inahitaji mabadiliko ili iweze kuendana na hari ilivyo sasa kwani kuna wanachama wengi wenye fedha ambazo zinaweza kuisaitia lakini wanashindwa kuwekeza kutokana na mfumo uliopo ambao unawanyonya zaidi bila kupata faida.

MWANACHAMA wa Yanga, Ridhiwani Kikwete amesema ili timu yao iingie katika mfumo mpya wa mabadiliko kama walivyofanya watani zao wa Simba ni lazima na muhimu kwa wanachama wote Jangwani waukubali uchaguzi wa mpito.

Simba imetoka kuchagua viongozi wake wapya mapema mwezi huu ikiingia kwenye mfumo wa kisasa wa klabu kuendeshwa kwa hisa badala ya wanachama, huku Yanga ikielekea kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi waliojiondoa. Akizungumza na Mwanaspoti, Ridhiwani alisema Yanga haikuwa na viongozi wa juu kwa muda mrefu kitendo ambacho kikatiba sio sahihi, hivyo kudai kilichoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya uchaguzi ni muhimu kikafuatwa ili mambo mengine yaendelee.

Alisema kama uchaguzi ulivyotangazwa wa kuhakikishwa nafazi ya Yusuf Manji (Mwenyekiti), Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti), Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi, Said Ameir na Hashim Abdallah (wajumbe) ni muhimu wakazifanyia uchaguzi huku akiweka wazi kuwa hata watakaochaguliwa watakuwa ni viongozi wa mpito kutokana na kuwa katika mchakato wa mabadiliko.

“Nasema viongozi wa mpito kwa vile nasi kama Yanga tunatamani kuingia katika mfumo wa hisa kama walivyo watani zetu Simba, kwa upande wetu inaturuhusu bila ya mabadiliko hivyo ni jambo jema kama tutamaliza hili suala la uchaguzi mapema na tukaanza mabadiliko,” alisema na kuongeza;

“Manji ametoka Yanga timu imeonekana kuyumba na kukosa hadi pesa za usajili bila ya baadhi ya wapenda Yanga kama Tarimba Abbas aliyejitolea kusajili baadhi ya wachezaji, timu isingeweza kufika hapo ilipo sasa hivyo tunatakiwa kutambua kuwa uendeshaji wa klabu unahitaji fedha na ili fedha zipatikana kitu kikubwa cha kukifanya ni mabadiliko,” alisema Ridhiwani.

Alisema hata huyo Manji wanayemng’ang’ania hawezi kuiendesha Yanga ikiwa katika mfumo huu wa sasa kwani anaweza kuchoka kutokana na kutumia fedha nyingi na hakuna anachokiingiza, ila kama watakubali kuingia mfumo wa hisa ni matajiri wengi watajitokeza kununua hisa na kuwekeza katika klabu hiyo kwani wanachokiingiza kitakuwa na faida kwao.