Rekodi zinambeba Juuko Simba

SIKU zote namba huwa hazidanganyi. Wakati mashabiki wa Simba wakiugulia kufuatia taarifa za kukosekana kwa nyota wao, Erasto Nyoni katika safu ya ulinzi, Juuko Murshid aliyetajwa kuchukua nafasi yake anaonekana kuwa mtu sahihi zaidi.

Nyoni aliumia kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM na bila shaka ataukosa mchezo wa kwanza wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Kukosekana kwake kumewapa presha mashabiki wa Simba, lakini juzi kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems amethibitisha kuwa Juuko ndiye atakayeziba nafasi yake.

Licha ya kwamba mara nyingi, Juuko alikuwa akiwekwa benchi lakini uzoefu wake na rekodi alizonazo kwenye michezo ya kimataifa inamfanya awe kitulizo sahihi cha mashabiki Simba.

Kupewa nafasi hiyo, ni wazi huenda mashabiki wasilione pengo la Nyoni, kwani Juuko ni bonge la beki wa kati anayejua kuifanya kazi zake kwa ufanisi na ataisaidia sana Simba, kwani amekabana na mastraika matata na hatari duniani bila presha.

REKODI ZILIVYO

Beki huyo kutoka Uganda, ni miongoni mwa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo alianza kulitumikia tangu ngazi za vijana.

Juuko, alianza kucheza timu ya taifa lake kwa vijana waliochini ya umri wa miaka 20 kwenye miaka ya 2011 hadi 2012 wakati huo, akiwa mchezaji wa Bunamwaya ya kwao Uganda.

Mwaka uliofuata (2013), Juuko aliyeondoka Bunamwaya kwa kujiunga na SC Victoria University, alichaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa tena kwa mara nyingine lakini safari hiyo, ilikuwa chini ya miaka 23.

Kufanya kwake vizuri akiwa na SC Victoria University, kuliifanya Simba SC kuhitaji huduma yake na mwishowe ikamsajili 2014.

Mara baada ya kutua Simba, beki huyo ambaye alizaliwa Entebbe, Uganda, Aprili 14, 1994 ndipo milango ilipoanza kufunguka ya kuanza kuitwa na kutumika The Cranes kwenye michezo mbalimbali ya kimataifa.

Mchezo wake wa kwanza mkubwa wa ushindi kwa Juuko upande huo wa soka la kimataifa akiwa na timu yake ya taifa la Uganda, ilikuwa Novemba 12, 2015 wa kuwania tiketi ya Kombe la Dunia lililofanyika mwaka jana kule Russia.

Juuko kwenye mchezo huo, alicheza kwa dakika zote 90 kwa kuwazuia ipasavyo, washambuliaji hatari wa Togo ambao alikuwa Ayite Jonathan aliyekuwa akiichezea Alanyaspor ya Uturuki na Dossevi Mathieu aliyekuwa Olympiakos Pirates.

Katika mchezo wa raundi ya pili, Uganda iliitandika Togo bao 1-0, lililofungwa na Miya Farouk na kwenye ule wa marudiano ikiwa nyumbani Uganda, Juuko alifanya vizuri kwa kuisaidia The Cranes kushinda mabao 3-0, hivyo kuitoa Togo kwa jumla ya mabao 4-0 na kuingia kwenye makundi.

TIKETI YA KOMBE LA DUNIA 2018

Mchezo mwingine mkubwa kwake ulikuwa ule wa Oktoba 7, 2016 pale Uganda ilipokuwa na kibarua cha kukabiliana na Ghana kwenye hatua ya raundi ya tatu ya kuwania nafasi ya kwenda Fainali za Kombe la Dunia 2018 Russia uliochezwa kwa mtindo wa makundi.

Vinara wa kila kundi kwenye makundi matano ndio waliopata nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika fainali hizo ambapo zilizoenda ni Tunisia, Nigeria, Morocco, Senegal na Misri.

Juuko alipambana na akiwa na Uganda yake kwenye Kundi E lililokuwa na vigogo kama vile Misri, DR Congo na Ghana na wakamaliza kwenye nafasi ya pili kwenye kundi hilo nyuma ya Mafarao ambao walifuzu kwenda Russia.

Katika hatua hiyo ya makundi mwaka jana, Juuko alipambana na washambuliaji wa Ghana aliyekuwa nahodha wao, Asamoah Gyan aliyekuwa akiichezea Shanghai SIPG F.C ya China na Jordan Ayew aliyekuwa Aston Villa ya England.

Kwenye mchezo huo, uliochezwa Oktoba 7, 2016 Juuko aliishia kuonyeshwa kadi ya njano, lakini hapakuwa na mshambuliaji yeyote wa Ghana aliyefunga bao kwenye mchezo huo ambao ulimalizika kwa suluhu.

Novemba 12, 2016 beki huyo alicheza kwa dakika 11 kwenye mchezo dhidi ya DR Congo na kupata majeraha, ambayo hayakumkwamisha kuikabili Misri, Agosti 31 ambapo walishinda kwa bao 1-0.

Juuko alikabiliana na mshambuliaji wa Liverpool kwenye mchezo huo, Mohamed Salah ambaye hakupata upenyo wa kufunga na badala yake alikuja kuonekana kwenye mchezo wa marudiano wa Septemba 5, 2017 kwa kufunga moja lililoipa ushindi wa Misri wa bao 1-0, jijini Cairo kwao Misri.

Ndani ya mwaka jana, Juuko amecheza michezo kadhaa mikubwa akiwa na The Cranes ambayo ni dhidi ya Cape Verde, Lesotho na Tanzania na kulisaidia taifa lake kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Afcon mwaka huu yatakayofanyika Misri.

AUSSEMS AMEPATIA

Kwa kumpa nafasi Juuko kuziba nafasi ya Nyoni amepata kwa mechi za Kundi D za Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Simba ikianza na Waalgeria kabla ya kuifuata AS Vita wiki ijayo katika mchezo wa pili, Kocha Partick Asseums amepata mtu sahihi.

Hata hivyo, kitu cha muhimu ni kuhakikisha beki huyo anapewa darasa mapema la kuwa mtulivu katika kuwakaba washambuliaji wa timu pinzani ili asiigharimu Simba.

Ndio, rekodi zinaonyesha Juuko ni moja kati ya mabeki ambao hawasiti kucheza faulo ili kuzuia mashambulizi na kujikuta akiangukia kwenye adhabu ya kadi na kuigharimu timu.

Juuko ni beki mbabe anayejua kudili na washambuliaji wakorofi, lakini kwa aina ya soka la timu za Kiarabu, kama atatumia mabavu na ubabe anaweza kuiponza Simba.