Rekodi za Simba zamtesa Ndayiragije

Muktasari:

Licha ya unyonge wa Azam katika mechi za Ligi Kuu, lakini timu hiyo imekuwa ikiitesa Simba katika mechi za Kombe la Kagame, ikiitungua mara mbili walizokutana ikiwamo fainali ya mwaka jana walipowacharaza mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

KESHO saa 1 usiku Simba na Azam wanatarajiwa kuvaana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020, lakini rekodi ya unyonge ikimtesa Kocha Etienne Ndiayiragije dhidi ya Wekundu wa Msimbazi.
Simba na Azam zitaumana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni pambano la pili kwao kukutana kwenye michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2001 kabla ya kusimama na kurejeshwa tena mwaka 2009.
Katika mchezo wao wa kwanza kukutana mwaka 2012, Simba iliitandika Azam kwa mabao 3-2, hivyo kufanya pambano la kesho kuwa mtihani mzito kwa Wanalambalamba ambao inanolewa na Kocha Ndayiragije ambaye hana rekodi nzuri kwa Vijana wa Msimbazi.
Kwa misimu mitatu tangu Mrundi huyo atue nchini na kuanza kuifundisha Mbao FC kabla ya kuhamia KMC msimu uliopita, hajawahi kuonja ushindi wowote mbele ya Simba ni mechi moja tu Ndayiragije aliambulia sare, lakini mechi nyingine tano zote amechezea.
Akiwa Mbao kwa misimu miwili, Ndayiragije alikutana na Simba mara nne, huku akipoteza mechi tatu kwa kulala 1-0, 3-2 na 5-0, huku mchezo mmoja ukiisha kwa sare ya 2-2, lakini akiwa na KMC msimu uliopita kocha huyo mbele ya Simba amenyooshwa nje ndani kwa kufungwa mabao 2-1 kila mechi.
Kwa rekodi hizo za Ndayiragije na zile za Azam mbele ya Simba ni wazi kocha huyo na vijana wake watakuwa na kibarua kizito cha kupindua meza mbele ya Wekundu hao wanaofundishwa na Patrick Aussems ambaye msimu uliopita alimburuza Mrundi huyo.
Licha ya rekodi hizo, lakini soka ni mchezo wa maajabu na kwa namna vikosi vyote vilivyofanya usajili kuimarisha vikosi vyao kwa msimu huu ni wazi pambano la kesho usiku litakuwa na upinzani, huku Azam ikitaka kulipa kisasi cha mwaka 2012 cha michuano hiyo.
Pia watataka kulipa kisasi cha msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara kwa kufumuliwa mabao 3-1, huku Meddie Kagere akitupia mabao mawili na John Bocco, nahodha wa zamani wa Azam akifunga bao jingine na Frank Domayo alifunga la kufutia machozi la Azam.
Kocha huyo amesisitiza kuwa, rekodi za nyuma hazimshughulishi na akili yake ni kuona katika mechi ya kesho anapata matokeo mazrui licha ya kukiri Simba ni moja ya timu ngumu nchini.
Timu hizo pia zitatumia mechi hiyo kama maandalizi ya kuelekea mechi zao za marudiano za michuano ya kimataifa, Simba ikijiandaa kuialika UD Songo ya Msumbiji aliotoka suluhu katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam ikitarajiwa kuipokea Fesil Kemena ya Ethiopia waliowatungua bao 1-0 ugenini katika Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi iliyopita.