Rekodi za Kocha Mpya Simba Mmh!

Muktasari:

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipata taarifa kocha huyo alishamalizana na Simba na ujio wake ulikuwa ni wa kusaini mkataba wa mwaka mmoja ili kuchukua nafasi ya Aussems na atasaidiwa na Seleman Matola aliyetangazwa siku moja kabla yake na wote leo watakuwa mazoezini Simba Mo Arena uliopo Bunju.

WIKI mbili tangu imtimue Patrick Aussems, mabosi wa Simba jana Jumatano wamemshusha na kumtangaza Kocha Sven Ludwig van den Broeck kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo na leo anatarajiwa kutambulishwa rasmi kwa wachezaji pamoja na wasaidizi wake mazoezini.

Kocha huyo, ambaye aliwasili nchini mchana jana na mabosi wake kufanya usiri mkuu, ni pendekezo la Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa kutokana na ujana alionao akiamini ataibeba Simba kwenye mechi za Ligi Kuu na Kombe la FA na michuano mingine waliyonayo kwa sasa.

Kocha huyo kutoka Ubelgiji kama ilivyokuwa kwa Aussems, ametoka kutimuliwa timu ya Taifa ya Zambia iliyoshindwa kwenda fainali za Afcon 2019 zilizofanyika Misri, ana miaka 40 kwani amezaliwa Septemba 22, 1979 na enzi za uchezaji wake alikuwa kiungo mkabaji katika timu kadhaa.

Miongoni mwa timu alizozichezea ni pamoja na Mechelen ya kwao Ubelgiji na klabu maarufu ya Uholanzi Roda JC kabla ya kugeukia ukocha katika klabu ya Niki Volou mwaka 2014 .

Awali, mabosi wa Simba walitangaza huenda kocha huyo angetua nchini Ijumaa, lakini Mwanaspoti lilinasa jamaa angetua saa 7 mchana wa jana na kuamua kutinga Uwanja wa Ndege na kumshuhudia akitolewa uwanjani hapo kwa geti maalumu na kuingizwa kwenye gari na kwenda kufichwa katika moja ya hoteli ya kitalii ya katikati ya jiji.

Kocha huyo alitua rasmi saa 9 alasiri kwa ndege ya Emirates na kupokewa na Mratibu wa Habari na Mitandao ya Kijamii, Rabi Hume pamoja na madereva wakuu wa klabu hiyo, Michael Omog na Mathew Shayo na jamaa, ambaye hakupatikana jina lake mara moja na kumtoa kwa siri bila Mwanaspoti kupata japo picha.

Baadaye Simba baada ya kushtukia Mwanaspoti limeshanasa taarifa za ujio wa kocha huyo, waliamua kwenda kumficha Serena na kutangaza kupitia mitandao yao ya kijamii kuwa, wangemtangaza kocha huyo rasmi saa 1:30 usiku japo hawakufanya hivyo kwa wakati kama walivyopanga.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipata taarifa kocha huyo alishamalizana na Simba na ujio wake ulikuwa ni wa kusaini mkataba wa mwaka mmoja ili kuchukua nafasi ya Aussems na atasaidiwa na Seleman Matola aliyetangazwa siku moja kabla yake na wote leo watakuwa mazoezini Simba Mo Arena uliopo Bunju.

Van den Broeck anakuwa kocha wa 21 tangu mwaka 1999, huku wengine wakijirudia mara kadhaa kama Abdallah Kibadeni, Milovan Cirkovic na Patrick Phiri.

NI NANI?

Sven Ludwig Vandenbroeck, alizaliwa Septemba 22, 1979 katika mji wa Vilvoorde, Belgium na alianza soka kama mchezaji mwaka 1996 alipotua Mechelen ya kwao hadi 2000 kabla ya kujiunga na Roda JC aliyoichezea mechi 55 na kufunga bao moja tu.

Mwaka 2004–05 alijiunga na De Graafschap aliyoichezea mechi 19, bila kufunga bao kama ambavyo alikwenda Akratitos 2005.

Pia mwaka 2006–07, alijiunga na Lierse kisha kutua Vise kisha kutua Løv-Ham ya Norway mwaka 2009.

Baadaye alihamia kwenye ukocha akianza kuinoaNiki Volou ya Ugiriki mwaka 2014 kama kocha wa muda.

Kisha akawa Kocha Msaidizi wa timu yua Oud-Heverlee Leuven na timu ya Taifa ya Cameroon iliyotwaa ubingwa wa AFCON 2017.

Julai mwaka jana alinyakuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Chipolopolo hadi Februari mwaka huu wakati Shirikisho la Soka la Zambia, walitangaza kutokuongeza mkataba kocha huyo aliokuwa na timu hiyo kwa mwaka mmoja tu.

Zambia waliamua kuvunja mkataba wa Van den Broeck, Machi 2019, kutokana na kushindwa kufuzu fainali za kombe la mataifa Afrika ambalo lilifanyika nchini Misri.