Refa Simba, AS Vita ni balaa!

Saturday March 16 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN

ACHANA na homa ya pambano la Simba na AS Vita linalopigwa baadaye leo Jumamosi pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mpango mzima ni mwamuzi wa mchezo huo, Noureddine El Jaafari.
Mwamuzi ambaye amepewa rungu na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuchezesha mchezo huo, ana miaka 40 na anaweza kukumbukwa kwa namna atakavyoamua mchezo huo muhimu.
El Jaafari, atakuwa akisaidiwa na waamuzi wa pembeni ambapo namba moja atakuwa Hicham Ait Abbou na namba mbili ni Yahya Nouali wote kutoka nchini Morocco.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi saba za mwisho ambazo El Jaafari amechezesha katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, ametoa kadi za njano 18 na nyekundu mbili. Mechi ya mwisho kuchezesha ilikuwa Machi 10 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Salitas ya Burkina Faso na Enugu Rangers ya Nigeria, ambapo matokeo yaliisha kwa sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huu El Jaafari alitoa kadi nne za njano na nyekundu moja kwa beki wa kati wa Enugu Rangers, Semiu Liadi.
Mechi nyingine alizochezesha ni Al Hilal waliochomoza na ushindi wa mabao 3–0 dhidi ya Al Ittihad, ambapo alitoa kadi moja ya njano kwa kwa beki wa Al Ittihad, Mahmoud Rizk.

Advertisement