Redondo: Ajibu anajua sana, basi tu

KIUNGO fundi wa mpira wa Biashara United, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ amefichua kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu anajua sana ila anapaswa kupambana kwelikweli Msimbazi awakalishe wageni wanaopewa nafasi kikosi cha kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Redondo aliyewahi kukipiga Msimbazi, alisema hashangazwi kuona Ajibu kukosa nafasi kikosi cha Simba kwa vile Wekundu hao wamejaza vichwa vya maana, hivyo ni lazima akomae licha ya kipaji kikubwa cha soka alichonacho kiungo huyo aliyeichezea pia Yanga.

Redondo alisema Ajibu kabla ya kurejea Simba alikuwa tegemeo ndani ya Yanga akiifungia mabao muhimu na hata kuongoza kutoka pasi za mabao na kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, hivyo ni lazima arejeshe makali yake kwani soka analijua na ana kipaji kikubwa.

Kiungo huyo wa zamani wa Azam, alisema kama akiwa Yanga alipambana na kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tena kwa kiwango bora kwani nini ashindwe akiwa Simba, hivyo anakiwa kujitambua na kujua yeye ni mchezaji mwenye uwezo mkuwa hivyo anatakiwa kupambania kipaji chake.

“Ajibu ni bonge la mchezaji na ana hadhi ya kucheza hizo klabu mbili kubwa kutokana na uwezo wake hivyo anatakiwa kupambana zaidi ili aweze kupata nafasi na kumthibitishia kocha kuwa ana kipaji,” alisema Redondo.