Real Madrid waambiwa Pogba watamsikia kwenye bomba

Muktasari:

Taarifa za kutoka Hispania zinaweka bayana kwamba Man United imeshaweka msimamo kwamba hawawezi kumuuza supastaa wao huyo kwa gharama yoyote ile ndani ya dirisha hili la uhamisho wa wachezaji la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Madrid, Hispania. Real Madrid wameambiwa waziwazi bila ya kificho na Manchester United kwamba wasahau kabisa suala la kumpata Paul Pogba kwenye dirisha la majira ya kiangazi kwa sababu wao hawapo tayari kumuuza hata kama itawekwa mezani ofa ya Pauni 185 milioni.

Pogba, aliyeshinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, amekuwa akifukuziwa na Real Madrid kwa muda mrefu katika dirisha hili la majira ya kiangazi huku mwenyewe akiwahi kukiri kwamba anataka kukumbana na changamoto mpya msimu huu.

Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane amekuwa akimtamani sana kiungo huyo akakipige kwenye kikosi chake, lakini sasa mambo yanaonekana kuwa magumu kwa sababu tayari wameshafanya usajili wa Pauni 280 milioni kunasa nyota wapya.

Taarifa za kutoka Hispania zinaweka bayana kwamba Man United imeshaweka msimamo kwamba hawawezi kumuuza supastaa wao huyo kwa gharama yoyote ile ndani ya dirisha hili la uhamisho wa wachezaji la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Dirisha la usajili huko England limeshafungwa tangu Alhamisi iliyopita, hivyo timu yoyote itakayouza kwa sasa haitakuwa na nafasi ya kumsajili mchezaji mwingine wa kuja kuziba pengo lake hadi Januari mwakani.

Baada ya kuondoka kwa wakali wawili wenye uzoefu mkubwa, Marouane Fellaini, aliyeondoka Januari kwenda China na Ander Herrera, aliyejiunga na Paris Saint-Germain kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, kocha wa Man United,Ole Gunnar Solskjaer amebaki na viungo wachache sana kwennye kikosi chake. Pogba na staa na nembo ya klabu hiyo, hivyo si kocha wala mabosi wa timu hiyo watakaokuwa tayari kumpiga bei huku ikiwa alicheza kwa kiwango bora kabisa katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea Jumapili iliyopita.