Real kumtoa Ronaldo kwa PSG kumnasa Neymar

Friday January 12 2018

 

Madrid, Hispania. Real Madrid imeanza kuweka nguvu za kutaka kumsajili Neymar mwaka 2019, kwa kumtoa Cristiano Ronaldo kwa PSG kama sehemu ya kukamilisha uhamisho huo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania.

Kurejea kucheza La Liga kwa nyota wa zamani wa Barcelona limekuwa ni jambo linalozungumza tangu alipoondoka kwa miamba hiyo msimu huu.

Gazeti la Marca limeripoti kuwa Real Madrid wanaamini 2019 ndiyo mwaka wa kukamilisha uhamisho huo, wanataka kuendeleza mahusiano mazuri na wammiliki Paris Saint-Germain.

Kuna sababu nyingi zinazofanya Real Madrid wajiamini katika kufanikisha usajili huo wenye historia ya utata zaidi.

Real Madrid ipo tayari kutumia zaidi ya pauni 178milioni kwa mchezaji huyo ambaye wakati huo atakuwa na miaka 28.

Pia, watakuwa tayari kumtoa Cristiano Ronaldo ambaye anaonekana anamapenzi na PSG kama sehemu ya uhamisho huo, hiyo ni ishara kuwa mshindi huyo wa Ballon d’Or mara tano siku zake zimeanza kuhesabika Madrid.

Real haijafanya usajili wa Galactico tangu walipomnunua James Rodriguez mwaka 2014. Kwa sasa wameweka nguvu katika kusajili vijana chipukizi kutoka Hispania.

Hata hivyo, kiwango kibovu kilichoonyeshwa na timu hiyo msimu huu imemfanya rais Florentino Perez kufikiri kuhusu kujenga upya kikosi chake.