Real Madrid kumrudisha Bale England

Muktasari:

  •  Kocha Zinedine Zidane amesema klabu hiyo itamtoa kwa mkopo, lakini atavuna Pauni10 milioni na mshahara wa Pauni250,000 kwa wiki. 

Rome, Italia. Real Madrid imempa ‘ofa’ mshambuliaji Gareth Bale kurejea Tottenham Hotspurs kwa mkopo katika usajili wa majira ya kiangazi.

Bale aliondoka Spurs kwenda Real Madrid mwaka 2013 na kuweka rekodi ya kununuliwa kwa Pauni 86 milioni.

Kocha Zinedine Zidane amesema klabu hiyo itamtoa kwa mkopo, lakini atavuna Pauni10 milioni na mshahara wa Pauni250,000 kwa wiki.

Spurs imetuma maombi ya kutaka kumrejesha mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Walas, baada ya kukosa mvuto kwa Zidane.

Mara kadhaa Zidane amekuwa akimtaka Bale kusaka klabu mpya ya kujiunga nayo kwa kuwa hana nafasi katika kikosi chake.

Licha ya Zidane kumuweka sokoni nyota huyo, hakuna klabu ya Ulaya iliyojitokeza kutaka huduma ya winga huyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Bale analipwa mshahara wa Pauni 600 kwa wiki, lakini Real Madrid imekubali kumtoa kwa mkopo kwa klabu ambayo itakubali kumpa mshahara wa Pauni250 kwa wiki na ada ya Pauni10 milioni.

Mchezaji huyo alicheza kwa kiwango bora Spurs akifunga mabao 21 katika Ligi Kuu England katika msimu wake wa mwisho kabla ya kutimkia Real Madrid. Bale ana mkataba unaomalizika mwaka 2022.