Ratiba kuamua ubingwa Man City, Liverpool EPL

Wednesday March 13 2019

 

By Fadhili Athumani

NI mechi nane tu. Ndio mehi nane ndo za kuamua bingwa wa Ligi Kuu England. Kama kuna kipindi watu huwa bize kufuatilia mechi za Ligi Kuu England, hiki ndo chenyewe.

Manchester City mabingwa watetezi wanauwaza ubingwa, Liverpool wanaokimbizana nao wanaomba dua Man City iteleze kidogo tu ifanye kweli baada ya kutaabika misimu kibao ikilisaka taji la Ligi Kuu England. Wana presha hasa.

Top Four vita inabaki kwa Tottenham, Arsenal, Manchester United na kwa mbaaali Chelsea. Hata hivyo, taji la Ligi Kuu vita ni ya wababe wawili tu, City ya Pep Guardiola na Liverpool ya Mjerumani Jurgen Klopp. City ikiongoza kwa alama zao 74 huku Liverpool wenye presha kubwa wakiwa na 73. Kazi ipo.

Hata hivyo, hatma ya City au Liverpool inayopambana kuvunja ukame wa mataji uliodumu kwa miaka 29, itategemea na ratiba yao ya mechi zilizosalia. Ni vita ya kufa mtu na mmoja lazima alie.

MAN CITY

Kwa sasa wanaongoza ligi, wakiwa na pointi 74, huku wastani wao wa kupata walau pointi, katika uwanja wa nyumbani na ugenini, ukiwa ni 1.33. Ratiba ya Man City, inaonesha, Machi 30, wanakutana na Fulham, ugenini.

Watakuwa wenyeji wa Cardiff City (Aprili 06), watasafiri kuifuata Crystal Palace (Aprili 14), watarudi Nyumbani, kuwavaa Tottenham (Aprili 20), Kabla ya kwenda Old Trafford kuumana na Mashetani wekundu (Aprili 24).

Baadaye City wataifuata Burnley (Aprili 28), wenyeji wa Leicester City (Mei 04), watarudi nyumbani kumaliza msimu huu na Brighton and Holve Albion (Mei 12).

Mabingwa hao watetezi, wataifuata Crystal Palace, na siku hiyo hiyo Liverpool watakuwa wenyeji wa Chelsea.

Mechi zote zitapigwa muda mmoja. Sawa na kilichotokea msimu wa 2013-14. Kama hiyo haitoshi, wakati Brendan Rodgers, akijiandaakulipiza kisasi, Leicester watazuru Etihad, macho na masikio yataelekezwa Old Trafford, kwenye Manchester Derby (Apili 24).

City wakishinda ni hasara kwa Liverpool, ila United akishinda itakuwa ni faida kwa Majogoo wa Jiji. Hiyo pia itamaanisha, Liverpool ambao wikendi ijayo watakuwa na kibarua dhidi ya Fulham ugenini, watakuwa na mechi moja mkononi, kwani City watakuwa na shughuli pevu ya kwenye kombe la FA.

Siku nne kabla ya kukutana na United, City watakuwa Etihad, kuwaalika Tottenham, kisha watakwenda Turf Moor, kuwavaa Burnley. Pointi sita ugenini dhidi ya Fulham na nyumbani dhidi ya Cardiff ni kitu kinachotarajiwa.

Mabingwa hao watetezi, watakuwa na matumaini makubwa kuwa, wabishi wa ligi msimu huu, Brighton watakubali kuogelea na sio kukaza kama ilivyo kawaida yao, maana kikosi cha Chris Hughton, wakati mwengine ni wabishi balaa, hasa wakiwa pale Amex.

LIVERPOOL

Hawa nao wana shida, kuna kipindi walikuwa wanaongoza ligi, wakiwa kileleni na tofauti ya pointi saba. Hivi sasa wameshushwa hadi nafasi ya pili. Tofauti ya pointi ni moja tu. Wastani wao wa kushinda mechi ugenini na nyumbani ni 1.32. wana pointi 73.

Ratiba yao inaonyesha Machi 17, watasafiri kuwafuata Fulham, halafu watakuwa wenyeji wa Tottenham (machi 31), kisha wawafuate Southampton (Mei 04). Watarudi nyumbani kuwavaa Chelsea (Aprili 14), kabla ya kwenda Cardiff (Aprili 21).

Aidha, Liverpool watakuwa na kibarua pale Anfield, dhidi ya Huddersfield (Aprili 26), halafu wataenda St. James Park, kuwavaa Newcastle United (Mei 04), baada ya hapo watarudi Anfield kumaliza mbio za ubingwa dhidi ya Wolvehampton Wanderers (Mei 12). Ukilinganisha pointi za ugenini na nyumbani ambazo Liverpool na Man City, wanaweza kuzipata katika mechi zilizosalia, tofauti ni 0.01. Tofauti hii ni kwa faida ya City, kwa lugha rahisi, Liverpool wana kibarua kigumu katika mbio hizi.

Liverpool anakabiliwa na mtihani wa kukutana na timu zinazopigana kuepuka kushuka daraja. Hii inaweza kuwapa kazi ngumu, maana anakutana na wafia maji, ambao kwa kawaida hawaishi kutapatapa. Fulham, Southampton na Cardiff, wanapambana kujinusuru huko mkiani. Wanahitaji pointi kwa gharama yoyote ile. Kwa upande wao, Newcastle wako katika kiwango kizuri na lazima watakuwa wabishi St. James Park.

Klabu mbili za ‘top six’, zitaenda Anfield kabla msimu haujaisha. Tottenham ya Mauricio Pochettino na Chelsea.

Kiwango cha Huddersield, ni cha mashaka. Vijana wa Jan Siewert, wako katika hatari ya kushuka daraja. Hata hivyo, kama kuna kitu kibaya kinachoweza kuwakumba Liverpool, ni kukutana na Wolverhampton Wanderers, katika dakika za mwisho za msimu.

TAFSIRI YAKE

Ni suala la mahesabu tu. Wakiwa na faida ya pointi moja na mechi laini kuliko wapinzani wao, ni dhahiri Man City wako hatua chache kutetea ubingwa wao. Kazi kubwa iko kwa Guardiola, ambaye lazima achange karate zake vizuri. Jurgen Klopp ana kila sababu ya kupambana. Mechi nane zilizosalia, ni lazima wapate ushindi, walau katika mechi tano. Wakati huo huo, waendelee kusali mchezo wa Manchester Derby, iende upande wa Man United. Vita ni Vita Muraa!

Advertisement