Ratiba kilio kwa nyota wa TZ Prisons

Dar es Salaam. Wachezaji wa Prisons, Salum Kimenya na Benjamini Asukile wameitaka Bodi ya Ligi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutumia busara kuzifiria timu ndogo kwani ratiba zinawachosha na kuwaumiza na kushindwa kuonyesha ubora wao uwanjani.

Wachezaji hao wamefunguka jambo hilo baada ya timu yao kutakiwa kucheza mechi mbili ndani ya siku tatu katika mikoa miwili tofauti.

Prisons itatakiwa kuikabili JKT Tanzania Oktoba 19 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kisha irudi Sumbawanga kucheza na Simba Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, ambao ndiyo wanautumia kwa sasa kama uwanja wao wa nyumbani.

Wakati Wajelajela hao wakijiandaa kcheza mechi mbili ndani ya siku tatu, wapinzani wao, Simba wenyewe kwa sasa wanafanya mazoezi pekee Dar es Salaam wakisubiri mechi hiyo ya Oktoba 22 kwani hawana mechi nyingine yoyote wiki hii.

Muda mfupi baina ya mechi hizo mbili ndiyo uliowaibua wachezaji hao ambao walisema ratiba hiyo haiko sawa kwao kwani inawaumiza hivyo Bodi ya Ligi wanatakiwa kutumia busara.

“Hizi ratiba zinatuumiza sana wachezaji yaani Bodi ya Ligi wawe wanangalia na kutuonea huruma maana ratiba kama hiyo hata muda wa kupumzika hatupati.

“Haiwezekani tucheze na JKT Dodoma halafu safari kurudi Sumbawanga kuwasubiri Simba, hivi kweli hata hiyo mechi tutaweza kuonyesha kiwango chetu?

“Naomba tu watumie busara katika hii ratiba,” alisema Asukile.