Rashford nje hadi mwisho wa msimu, kuikosa Euro 2020

Muktasari:

Majeraha ya Rashford yanaongeza majanga kwenye kikosi cha England na kumuacha katika wakati mgumu Kocha Gareth Southgate ambaye tayari ana dalili za kumkosa straika wa Tottenham, Harry Kane ambaye ni majeruhi.

MANCHESTER, ENGLAND . NDIO basi tena! Ndiyo neno rahisi unaloweza kulitumia baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa straika tegemeo wa Manchester United, Marcus Rashford atakaa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu na kuna kila dalili za kuikosa pia michuano ya Euro 2020.

Kwa mujibu wa Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer, Rashford atakaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya mgongo yanayomsumbua.

 Solskjaer amedai jeraha la Rashford ni kubwa kuliko lilivyotabiriwa awali na sasa atakaa nje kwa kipindi kirefu zaidi ya kilichotarajiwa.

Majeraha ya Rashford yanaongeza majanga kwenye kikosi cha England na kumuacha katika wakati mgumu Kocha Gareth Southgate ambaye tayari ana dalili za kumkosa straika wa Tottenham, Harry Kane ambaye ni majeruhi.

England itacheza mechi yake ya kwanza ya michuano ya Euro 2020, Juni 14, mwaka huu dhidi ya Croatia na kwa mujibu wa Solskjaer, Rashford anaweza asiwe fiti kuiwahi michuano hiyo.

Solskjaer, ambaye usiku wa kuamkia leo Ijumaa aliiongoza timu yake kwenye pambano la Europa League dhidi ya Club Brugge, alisema: “Marcus (Rashfor) atakuwa nje kwa miezi kadhaa.

“Amefanyiwa vipimo na jeraha ni kubwa kuliko tulivyodhani awali. Natumaini atacheza msimu huu kabla haujaisha na kama hilo likitokea itakuwa katika mechi za mwisho kabisa za msimu.

“Itachukua muda, mimi si daktari nilikuwa natamani apone haraka lakini hali ni tofauti sasa.”

Rashford, 22, ambaye amekuwa akivaa kifaa maalumu mgongoni kumsaidia kuweza kutembea. Aliumia kwenye mchezo dhidi ya Norwich, Januari 11, kisha akajitonesha siku nne baadaye baada ya kuingia uwanjani kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Wolves.

Awali majeraha yake yalitarajiwa kumuweka nje kwa wiki sita, lakini sasa mambo yanaonekana kubadilika na atakaa nje kwa muda mrefu zaidi.

Solskjaer amekiri alikosea kumuingiza kwenye pambano dhidi ya Wolves, lakini anadai Rashford mwenyewe alikomaa kutaka kucheza mechi hiyo akidai alikuwa fiti.

Solskjaer alisema: “Alikuwa fiti kabisa siku chake kabla ya tukio la kuumia na mimi si daktari wa kujua kama hakuwa vizuri, hivyo sikujua kama alihitaji muda zaidi kupona kabisa.”

Majeraha ya Rashford si pigo kwa Man United pekee, bali hata England italazimika kutafuta mbadala wake Euro.