Rashford akaa anga za wababe Ulaya

Muktasari:

Staa Rashford atafikisha umri wa miaka 22, Oktoba 31 mwaka huu, lakini tayari ameshaweka mpira kwenye kamba mara 47 katika mechi za klabu, jambo linalomfanya awe amelingana na Ronaldo

MANCHESTER, ENGLAND.FOWADI wa Manchester United, Marcus Rashford amefunga mabao mengi kabla ya kutimiza miaka 22, huku akimfunika Raheem Sterling na kukaa kwenye anga moja ya supastaa wa dunia, Cristiano Ronaldo.

Hata hivyo, moto wote wa kufunga wa Rashford ni cha mtoto kwa Romelu Lukaku, ambaye kabla ya kufikisha umri wa miaka 22, tayari alikuwa ameshaweka mipira nyavuni mara 93.

Staa Rashford atafikisha umri wa miaka 22, Oktoba 31 mwaka huu, lakini tayari ameshaweka mpira kwenye kamba mara 47 katika mechi za klabu, jambo linalomfanya awe amelingana na Ronaldo. Kutoka sasa hadi Oktoba, Rashford bado ana nafasi ya kufunga zaidi na pengine kumzidi staa mwenzake wa Man United, Anthony Martial, ambaye alifunga mabao 48 kabla ya kutimiza umri wa miaka 22.

Straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amefunga mabao 52 wakati anatimiza umri wa miaka 22, hivyo Rashford anahitaji kufunga mara sita kabla ya kufika Oktoba 31 kuvunja rekodi hiyo ya Mwingereza mwenzake.

Takwimu zinaonyesha kwamba Lukaku amewafunika mastaa wengi akiwamo Lionel Messi kwa kufunga mabao mengi kabla ya kufikisha umri wa miaka 22, ambapo Mbelgiji huyo aliweka kwenye nyavu mara 93, huku Messi akifunga mabao 80, moja nyuma ya Wayne Rooney, aliyekuwa amefunga mara 81 kabla ya kufikisha umri wa miaka 22. Kane amefunga 52, Martial mara 48 huku Sterling akiwa amefunga mara 39

Kwa kumlinganisha na Kane, Rashford ambaye Julai mwaka huu alisaini dili matata huko Old Trafford linalomshuhudia akilipwa Pauni 300,000 kwa wiki, amefunga mara 29 kwenye Ligi Kuu England, sita kwenye Kombe la FA,  matano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, manne kwenye Europa League na matatu kwenye Kombe la Ligi, wakati Kane amefunga 24 kwenye Ligi Kuu, tisa kwenye Championship, sita kwenye Europa League, matano kwenye League One, manne kwenye Kombe la Ligi na mawili kwenye Kombe la FA, huku mawili mengine alifunga kwenye kufuzu Europa League.