Rashford achanganya watu huko United

Muktasari:

Akizungumza na Premier League Productions, Hargreaves alisema anatia shaka kama Rashford ana uwezo wa kuziba pengo kwenye fowadi lililoachwa wazi na Romelu Lukaku, aliyetimkia zake Inter Milan.

MANCHESTER, ENGLAND.MASTAA wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes na Owen Hargreaves wamesema wanachanganyikiwa, hawafahamu ni nafasi gani ya uwanjani ni bora kucheza Marcus Rashford kwa sababu kote anakopangwa anavurunda tu kama alivyofanya Jumamosi iliyopita kwenye kipute dhidi ya Southampton kwenye Ligi Kuu England.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ameanza msimu vizuri kwa kufunga mabao mawili na kuasisti katika mechi mbili za kwanza za Man United walizocheza dhidi ya Chelsea na Wolves.
Lakini, baada ya hapo, Rashford amekuwa hana maajabu ndani ya uwanja, akikosolewa kila kona baada ya kushindwa kuziba pengo kwenye nafasi ya ushambuliaji ikiwamo kucheza soka la kiwango cha hovyo kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Southampton uwanjani St. Mary's wikiendi iliyopita.
Akizungumza na Premier League Productions, Hargreaves alisema anatia shaka kama Rashford ana uwezo wa kuziba pengo kwenye fowadi lililoachwa wazi na Romelu Lukaku, aliyetimkia zake Inter Milan.
"Ni aibu kwa sababu nampenda sana Rashford kama mchezaji, amekuwa vizuri, lakini ukweli nadhani Man United wanahitaji Namba 9 mwingine," alisema Hargreaves.
"Sanchez ameondoka, Lukaku ameondoka, wanamhitaji aonyesha mambo. Martial amechukua namba 9, jambo zuri lakini, duh. Rashford alipata nafasi nyingi dhidi ya Southampton hakuzitumia. Ni kweli namba 9 kama anataka kucheza kutokea upande wa kushoto? Hawezi."
Gwiji mwingine wa Man United, Scholes amekubaliana na Hargreaves, akisema anadhani Rashford anahitaji kujionyesha wazi kwamba yeye ni mchezaji wa aina gani, sehemu gani anakuwa bora.
Scholes alisema: "Nadhani ni swali kubwa – yeye ni nani hasa? Ni kama Greenwood, Martial, au, yeye ni nani. Kwenye ile mechi dhidi ya Southampton, hakuonekana kabisa kama ni mshambuliaji wa kati. Sawa si vizuri kumjadili mtu baada ya mechi moja, lakini mimi namwona kuwa ni mfungaji wa mabao mahiri, lakini si mfungaji mahiri wa mabao."
Rashford kwa sasa yupo kwenye majukumu ya timu yake ya taifa ya England, ambako anatumaini ataongezea akaunti yake ya mabao ambapo kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate kitakuwa na shughuli ya kuzikabili Bulgaria na Kosovo kwenye mchakamchaka wa kufuzu Euro 2020.