Raptors yabeba taji la kwanza NBA

TIMU ya mpira wa kikapu ya Toronto Raptors, leo Ijumaa alfajiri imetwaa ubingwa wa ligi ya kikapu maarufu duninai ya NBA baada ya kushinda michezo 4-2 dhidi ya Golden State Warriors.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Toronto kutwaa ubingwa wa NBA tangu ilipoanzishwa mwaka 1995 kutokana na upanuzi wa ligi ya NBA na kuongezeka timu hiyo kutoka Canada.
Toronto Raptors yenye wachezaji wengi ambao sio raia wa Marekani (wachezaji wa Kimataifa) imeshuhudia mchezaji wa Cameroon, Pascal Siakam akifunga pointi 26 na kudaka rebounds 10, Kyle Lowry akiongeza pointi 26 na Kawhi Leonard akifunga pointi 22 huku ikiifunga Golden State Warriors pointi 114-110 katika mchezo wa sita wa fainali hizo za NBA.
Mchezaji mwenye asili ya Congo DRC, Serge Ibaka alimaliza mchezo na pointi 15.
Historia nyingine iliyoandikwa ni kuwa, Rais wa Toronto Raptors, Masai Ujiri ambaye ni raia wa Nigeria, amekuwa ni kiongozi wa kwanza wa Menejimenti ya timu yoyote ya NBA kutokea Afrika kutwaa ubingwa huo.
Kama haitoshi kuna damu ya Kiafrika ya kutosha inayochuruzika ndani ya Toronto Raptors ikimhusisha Masai Ujiri (Rais; Nigeria), Patrick Engelbrecht (Mkurugenzi wa mahusiano ya Kimataifa na msaka vipaji wa kimataifa; USA, South Africa); Patrick  Mutombo (kocha msaidizi; DRC); Jama Mahlalela (kocha mkuu wa Raptors 905; Swaziland); na wachezaji Pascal Siakam (Cameroon), Serge Ibaka (Congo), OG Anunoby (UK; Nigeria).
Kawhi Leonard ni mshindi wa mchezaji mwenye thamani zaidi kwenye fainali za NBA, tuzo inayofahamika kama Bill Russell NBA Finals Most Valuable Player Award.
Kawhi anaungana na wachezaji Kareem Abdul-Jabbar na LeBron James kuwa wachezaji pekee walioshinda tuzo hii mara mbili au zaidi na timu mbili tofauti. Kawhi alitwaa tuzo hii akiwa na klabu ya San Antonio Spurs mwaka 2014.
Nick Nurse ni kocha wa tatu katika misimu mitano iliyopita kushinda ubingwa wa NBA kama kocha mkuu wa timu akiwa katika mwaka wake wa kwanza, akiungana na Stev Kerr aliyefanya hivyo na Golden State mwaka 2015 na  Tyronn Lue akiwa na Cleveland Cavaliers mwaka 2016.