Ramos amponda kinoma Ronaldo

Muktasari:

  • Basi bana, nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos amefunguka na kumtaja yule ambaye anastahili kubeba tuzo hiyo, lakini akimkinjia kwenye maji, supastaa wa Ureno na Juventus, Ronaldo.

MADRID, HISPANIA. SI unajua ile orodha ya wakali wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka inayotolewa na Fifa imebakiza mastaa watatu tu kwa sasa wanaochuana, Cristiano Ronaldo, Mohamed Salah na Luka Modric?

Basi bana, nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos amefunguka na kumtaja yule ambaye anastahili kubeba tuzo hiyo, lakini akimkinjia kwenye maji, supastaa wa Ureno na Juventus, Ronaldo.

Wakati wengi wakimpa nafasi fowadi huyo wa zamani wa Los Blancos atabeba tuzo hiyo, Ramos amekuwa na mawazo tofauti na kusema mshindi anayestahili ni Luka Modric.

"Pengine kuna wachezaji wana nguvu kubwa sokoni na wana majina makubwa, lakini Modric ndiye anayestahili kubeba tuzo hiyo," alisema Ramos.

"Acha tusubiri tuone atakayeshinda. Ni rafiki yangu, lakini staa mkubwa pia. Ni aina ya wachezaji wachache ambao kama watashinda basi inakuwa furaha kwa wote kama itakavyokuwa kwao binafsi."

Modric ameshinda idadi sawa na mataji aliyoshinda Ronaldo msimu uliopita, lakini kiungo huyo wa Croatia kitu cha ziada kwake  alifika fainali ya Kombe la Dunia 2018 na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.