Ramos afunguka kuhusu kocha wa Real Madrid

Muktasari:

Nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos amesema, kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia suala la kufutwa kazi kwa kocha wao mkuu, Julen Lopetegui  licha kuwa wanapata matokeo mabaya ni vizuri wachezaji wenyewe wakatambua majukumu yao.

MADRID, HISPANIA. BEKI wa kati wa Real Madrid, ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo, Sergio Ramos amesema ni mapema mno kuanza kuzungumzia habari za kumfuta kazi Kocha Julen Lopetegui.
Real Madrid hali yao ni mbaya baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika mechi nne za karibuni, lakini mbaya zaidi ikishindwa kupata bao lolote katika mechi hizo.
Juzi Jumamosi ilichapwa na Alaves kwenye La Liga, kikiwa ni kichapo cha pili mfululizo na jambo hilo linakiweka rehani kibarua cha Lopetegui.
"Wakati mwingine ni bora kubadili kocha, lakini wakati mwingine si jambo zuri. Lakini, kwa hili la sasa ni mapema sana kuanza kuzungumzia kocha kwa sababu kila kitu kipo mikononi mwa wachezaji," alisema Ramos baada ya mechi hiyo ya kipigo.
"Watu wanazungumzia kufanyike uamuzi huo, lakini siyo jambo zuri kubadili kocha, itakuwa uchizi. Sisi wachezaji ndio watu wa kwanza kufahamu tunapaswa kuboresha viwango vyetu na hicho ndicho tunachotaka kufanya, tunalifahamu hilo.
"Kama kuna mtu anaona Real Madrid haitafanya lolote msimu huu, basi atakuwa amepotea. Tunapaswa kuwa na imani."