Ramani ya ubingwa Bara

Muktasari:

Nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amesema timu hiyo ikishinda viporo vyake tafsiri ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga ni kupishana pointi sita kwa mbili, akiwa na maana ya sare mbili za Wanajangwani na Msimbazi zipo tatu na kupoteza mchezo mmoja.

TAYARI Yanga imeshadondosha pointi tano katika mechi 20 huku watani zao wakipoteza sita mpaka sasa katika michezo yao 14, jambo ambalo limetafsiriwa na wataalamu wa soka ni kama vile ramani ya ubingwa Bara imefichwa kimtindo.

Kupotea kwa pointi tano za Yanga inayomiliki pointi 53 kileleni mwa Ligi Kuu Bara, kumetokana na sare mbili dhidi ya Simba, Ndanda na kupoteza dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’, Simba ilizidondosha kwa sare tatu na Yanga, Lipuli na Ndanda huku ikifungwa na Mbao FC.

Beki wa zamani wa Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema mzunguko wa ligi ungekuwa kama misimu iliopita iliokuwa na timu 16, ilipofikia Yanga ingekuwa na nafasi kubwa ya ubingwa ila kwa sasa bado ina kazi ngumu.

“Mechi za msimu huu ni nyingi kuna wachezaji kuchoka, mkoani kugumu hivyo lolote linaweza kutokea, Simba inapaswa kupambana kwa hali na mali ili viporo vyake visichache.

“Kiufundi huwezi kusema Simba ama Yanga ndio mabingwa ila kishabiki ni rahisi kusema hivyo, wachezaji watakaopambana ndio watafanya mashabiki wao waishi kwa furaha mwaka 2019, ila ukweli ramani ya ubingwa bado imefichwa kwa sasa,” alisema.

Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ nyota wa zamani wa Msimbazi alisema timu hiyo ikishinda viporo vyake tafsiri ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga ni kupishana pointi sita kwa mbili, akiwa na maana ya sare mbili za Wanajangwani na Msimbazi zipo tatu na kupoteza mchezo mmoja.

“Ikitokea Simba ikashinda viporo kisha ikaanza vizuri mzunguko wa pili itachangamsha na kuleta presha ya ushindani na itakuwa ngumu kujua bingwa ni nani,” alisema.

Naye staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema ni mapema kutabiri bingwa kutokana na mzunguko mrefu wa ligi na kudai timu za juu zina nafasi ya kutwaa taji hilo.