MTU WA PWANI : Ramadhan Kabwili,Yanga hawakugeuza sarafu

Muktasari:

Lakini mbali na mapendekezo ya benchi la ufundi, kigezo cha uzoefu wa kucheza kwenye timu za taifa kingewapa faida kubwa Shikalo na Metacha mbele ya Kabwili katika msimu unaokuja.

KWENYE dirisha kubwa la usajili, kipa Ramadhan Kabwili aliamua kuendelea kubakia kwenye klabu yake ya Yanga.

Kwa kuamua kwake kubaki maana yake kuna uwezekano mkubwa akawa kipa chaguo la tatu nyuma ya Mkenya, Farouk Shikalo na Metacha Mnata ambaye amejiunga na Yanga akitokea Bandari FC ya Kenya.

Kuna uwezekano finyu kwa Kabwili kuwa kipa chaguo la kwanza mbele ya Shikalo au chaguo la pili mbele ya Mnata kwa sababu wawili hao wamesajiliwa kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la ufundi chini ya Kocha Mwinyi Zahera.

Hadi Zahera anaamua kuwasajili Mnata na Shikalo maana yake hakuridhishwa na kiwango cha Kabwili na kipa mwingine aliyeonyeshwa mlango wa kutokea na klabu hiyo, Klaus Kindoki Nkizi.

Hali ingekuwa mbaya zaidi kwa Kabwili iwapo Yanga ingeamua kubaki na Kindoki ambaye jina lake limekatwa kwenye dakika za mwisho za usajili ili kumpisha mshambuliaji, David Mulinga.

Lakini mbali na mapendekezo ya benchi la ufundi, kigezo cha uzoefu wa kucheza kwenye timu za taifa kingewapa faida kubwa Shikalo na Metacha mbele ya Kabwili katika msimu unaokuja.

Shikalo ni kipa wa Timu ya Taifa ya Kenya ambaye aliweza kuwemo kwenye kikosi cha nchi hiyo ‘Harambee Stars’ kilishiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kama ilivyo kwa Metacha ambaye naye alikuwemno kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kilichokuwepo kule Misri kwenye fainali hizo.

Kama alishindwa kuwa chaguo la kwanza au la pili pindi Yanga ilipokuwa na makipa Beno Kakolanya na Kindoki, haiwezi kuwa rahisi kwake kuchomoza mbele ya Metacha na Shikalo.

Wengi tulitegemea kuona katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa la usajili, Kabwili angeondoka Yanga hata kwa mkopo kwenda klabu nyingine ili akapate nafasi ya kucheza kuliko kuendelea kubakia mahali ambako hapati nafasi hiyo.

Kuna pande mbili za faida na hasara kwa Yanga na Kabwili mwenyewe kutokana na uamuzi wa kipa huyo kuamua kuendelea kubakia kwenye timu yake.

Kwa Kabwili kubakia, maana yake ana uhakika wa kulipwa vizuri mishahara na posho pamoja na kupata huduma nyingine za hadhi ya juu ambazo huwa nadra kwa wachezaji wa timu nyingine kupatiwa.

Lakini kwa Yanga wanaendelea kuwa na uhakika wa wigo mpana wa idara ya kipa na hawana hofu kwamba hata Metacha na Shikalo wakiumia au kukosekana wana uhakika wa kuwa na kipa anayeweza kulinda vyema milingoti mitatu ya lango lao.

Kwa bahati mbaya inaonekana Kabwili na Yanga kila upande ulishindwa kutazama hasara za kipa huyo kuendelea kubakia kikosini kwenye msimu ujao.

Kutokana na kuwepo kwa uwezekano mkubwa kwa Kabwili kuwa chaguo la tatu msimu ujao, ni wazi kwamba yupo kwenye hatari ya kuporomosha kiwango chake kwani hatopata nafasi ya kutosha ya kucheza.

Kwa umri wake mdogo alipaswa kupata nafasi kubwa ya kucheza ili azidi kukomaa na kupata uzoefu wa kutosha ambao siku za usoni ni mambo ambayo yangekuwa na faida kwake.

Hataweza kuvipata kwa kusotea benchi na hiyo inaweza kumvuruga na kuathiri kipaji chake ambacho kilianza kuwapa matumaini wengi kuwa kitamfanya awe mmoja kati ya makipa bora hapa nchini na Afrika kwa siku za usoni.

Lakini kwa Yanga, kitendo cha kubaki na Kabwili maana yake kinafunga milango kwa makipa kutoka kwenye kikosi chao cha vijana kupata nafasi kwenye kikosi cha wakubwa.

Mara kwa mara nafasi ya kipa chaguo la tatu inapaswa kuwa ya kipa aliyepo kwenye kikosi cha vijana ili iwe fursa kwake kuanza kupata uzoefu na kujifunza lakini ni tofauti na Kabwili ambaye tayari alishapata nafasi ya kucheza hivyo inakuwa ni kama anajirudisha nyuma.

Pamoja na hilo, Yanga maana yake itaendelea kutumia gharama kubwa kumlipa mishahara na posho pia kumhudumia Kabwili ambazo ingeweza kuziepuka au kuzipunguza kwa kumtoa kwa mkopo au kumuuza timu nyingine.

Hili limekuwa likifanywa na klabu nyingi duniani kwa lengo la kulinda vipaji vya vijana wenye umri mdogo kama Kabwili na mara kwa mara limekuwa likizaa matunda.

Kwa bahati mbaya, Yanga na Kabwili mwenyewe kila upande unalitazama jambo hili katika upande wa faida tu pasipo kuangalia ule mwingine wa hasara jambo lililopelekea uamuzi wa kipa huyo kuendelea kubakia klabuni.

Kila upande ungetazama upande wa pili wa shilingi, pengine leo Kabwili angekubali kutolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine.