Raktic atangaza kuondoka Barca

Muktasari:

  • Mkataba wa sasa wa Rakitic unatarajia kumalizika Juni, 30 mwaka 2021, huku thamani yake katika soko la usajili ikiwa ni Euro 20 milioni.

BARCELONA, HISPANIA. KIUNGO wa klabu ya FC Barcelona, Ivan Rakitic amefichua  kuwa anafikiria kuondoka na kutafuta timu nyingine, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, baada ya kuona hayuko kwenye mipango ya muda mrefu ya klabu hiyo.

 Mkataba wa Rakitic unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu ujao na Barcelona wameripotiwa kuwa tayari kumuuza katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, ili kuepuka asiondoke bure pindi mkataba wake utakapomalizika mwakani.

Tetesi zinadai kuwa Rakitic anawaniwa na klabu mbalimbali kama vile Atletico Madrid, Napoli, Villarreal, Juventus, Sevilla,  Manchester United na Tottenham.

Kiungo  huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye tokea ajiunge na Barcelona mwaka 2014, amefanikiwa  kushinda mataji 13 alisema kuwa anadhani sasa ni wakati wa kusaka maisha kwingine badala ya kuendelea kubakia Barcelona.

“Pindi mchezaji anaposaini mkataba na klabu fulani, lazima atimize vile vipengele kwenye mkataba huo. Shauku yangu mimi ni kuhitaji kucheza jambo ambalo linanifanya nitafute sehemu nitakayopata nafasi hiyo.

 Nilihitaji mtu kutoka Barcelona aje na kusema hadharani kwamba bado wana  nihitaji na nitaendelea kubaki klabuni hapo mpaka mwisho wa mkataba wangu, lakini hilo silioni jambo linalofanya niwe tayari kuitumikia timu yeyote  itakayohitaji  saini yangu,” alisema Rakitic.

Sevilla ndio wanaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kumnasa Rakitic  wakitumia ushawishi wa familia yake kama ambavyo mwenyewe amekiri.

" Mimi na familia yangu tunaweza kwenda kuishi Sevilla muda sio mrefu, haraka iwezekanavyo ama baadae yote yanawezekana,” alisema Rakitic.

Rakitic alisajiliwa Barcelona kutoka Sevilla Julai, 2014, kwa ada ya uhamisho ya Euro 18 milioni.