BMT: Rais wa ngumi za kulipwa atarejea madarakani baada ya miezi sita

Muktasari:

Anea alichaguliwa kuwa rais wa TPBRC, Machi 31 mwaka jana katika uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kupata kura 109 dhidi ya 12 za mpinzani wake, Ally "Champion" Bakari.

Dar es Salaam.Wakati baadhi ya wadau wa ngumi za kulipwa wakiibua minong'ono kuhusu rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Joe Anea kupumzika kwa miezi sita kiutendaji, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema hakuna kipingamizi kwa Joe kupumzika kipindi hicho kisha kurejea kuendelea na majukumu yake.

Hivi karibuni wadau baadhi wa ngumi za kulipwa waliibua minong'ono wengine wakitaka kiongozi huyo ajiuzulu nafasi hiyo ili kupisha wengine waendelee, baada ya kuomba kuwa nje kwa matatizo ya kiafya.

Msitha amesema Anea atarejea madarakani baada ya miezi sita kupita kama alivyoomba apewe mapumziko katika kipindi hicho kwa masuala ya kiafya.

"Baraza limeridhia ombi hilo na baada ya miezi sita kupita atarejea kuendelea na majukumu yake ya kiutendaji kama alivyoomba," alisema Msitha.

Majukumu ya Anea sasa yatafanywa na makamu wa rais wa TPBRC, Agha Peter 'Mnazarethi'.

Makamu wa Rais wa TPBRC, Aga Peter alisema kuwa ataendelea kukaimu nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba na kuomba wadau kuendelea kutoa ushirikiano.