Rais wa PSG kikaangoni kwa tuhuma za rushwa

Muktasari:

Al-Khelaifi ni Mwenyekiti wa Kampuni ya beIN, anashtakiwa kwa kosa la kumshawishi Valcke kutenda kosa la jinai na kutoa rushwa.

PARIS, UFARANSA . RAIS wa Paris Saint Germain, Nasser Al-Khelaifi ameshtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa kwa katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jerome Valcke ili kupata haki za televisheni.

Mbali na Al-Khelaifi, Valcke pia ameshtakiwa kwa kosa la kupokea rushwa kwenye ishu ya haki za televisheni za Kombe la Dunia, ili kuipa nafasi Kampuni ya Televisheni ya beIN Media Group.

Al-Khelaifi ni Mwenyekiti wa Kampuni ya beIN, anashtakiwa kwa kosa la kumshawishi Valcke kutenda kosa la jinai na kutoa rushwa.

Taarifa iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Uswiss, Valcke ni mtuhumiwa kwa kwanza katika kesi hiyo anatuhumiwa kwa kupokea rushwa, kwa makosa ya jinai na kutoa nyaraka za uongo. Valcke alifungiwa kujihusisha na soka kwa miaka 12, baada ya kukutwa na hatia ya kuuza tiketi za magendo za Kombe la Dunia, kutumia vibaya gharama za usafiri, na jaribio la kuuza haki za televisheni kwa bei ya chini na kuharibu ushahidi.