Rais Magufuli awapa mzuka Waandishi wa michezo

Muktasari:

  • Shughuli za michezo zitarejea rasmi kuanzia Juni Mosi mwaka huu baada ya kusimamishwa tangu Machi 17 kama moja ya hatua za kukabiliana na virusi vya Corona.

Kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ya kuruhusu kurejea kwa shughuli za michezo, Juni Mosi imewapa mzuka waandishi wa habari za michezo nchini.
Katika kuhakikisha wanaunga mkono kauli hiyo Waandishi hao wameamua kuwa na mechi ya wenyewe kwa wenyewe ambayo itachezwa Jumapili ya Mei 31 katika uwanja wa Shule ya Sheria, Ubungo Mawasiliano jijini.
Mechi hiyo itakuwa ni baina ya waandishi wa habari za michezo walio kwenye ndoa na wale ambao hawako kwenye ndoa.
Katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 4:00 asubuhi mgeni rasmi atakuwa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao.
Kidao ataambatana na kocha mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, Oscar Mirambo.
Mdhamini wa mechi hiyo, Sweddy
Mkwabi aliyetoa jezi kwa kila timu amesema amefanya hivyo ili kuunga mkono juhudi zao za kuendeleza michezo.
"Naunga mkono jambo hili la mechi ya Waandishi hawa wa habari na siku ya mechi nitakuwepo uwanjani na na imani naweza kuongeza mchango wangu mwingine," anasema Mkwabi.
Mwandishi na mchambuzi wa michezo nchini, Shaffih Dauda alisema kwa upande wake ametoa zawadi ya Kombe ambalo itapewa timu itakayoshinda.
"Nadhani hili kombe ambalo nimelitoa linaweza kubaki hapa hapa dukani kwani naamini timu yangu ya Wenye ndoa tunaweza kushinda," anasema Dauda.