Raiola azidisha chokochoko, kisa Pogba ang’oke Manchester United

Muktasari:

Maneno hayo ya Raiola yamekuja siku chache baada ya Solskjaer kusema hatakubali kupelekeshwa na Raiola na kwamba, Pogba ni mchezaji wake na yeye pamoja na uongozi wa timu hiyo ndio wataamua cha kufanya.

WAKALA wa Paul Pogba, Mino Raiola ameendeleza vita ya maneno dhidi ya Manchester United safari hii akimshukia kocha wa timu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer huu ukiwa ni mwendelezo wa harakati zake za kumng’oa mteja wake Old Trafford.

Raiola ambaye anafanya kila njia kuhakikisha anafanikisha dili la mteja wake kurudi Juventus, amemchana Solskjaer kwa kumwambia kuwa Pogba sio mfungwa na hamilikiwi na mtu yeyote pale United.

Maneno hayo ya Raiola yamekuja siku chache baada ya Solskjaer kusema hatakubali kupelekeshwa na Raiola na kwamba, Pogba ni mchezaji wake na yeye pamoja na uongozi wa timu hiyo ndio wataamua cha kufanya.

Lakini, Raiola amedai kuwa kocha huyo ana ‘stresi’ ndio maana haelewi anachozungumza na kuwa Pogba sio mfungwa wala mtumwa wa mtu kwani anaweza kuamua chochote kwa sababu ni haki yake kufanya hivyo.