Raiola asema De Ligt kaenda PSG ni uongo mtupu

Muktasari:

Mapema wiki hii kulikuwa na taarifa kwamba PSG imeweka mambo sawa kwenye kumnasa staa huyo huku ikiripotiwa itamlipa mshahara wa Pauni 211,000 kwa wiki.

MILAN, ITALIA.WAKALA mjanja, Mino Raiola amerudisha matumaini kwa timu kibao zinazomsaka beki wa kati wa Ajax, Mdachi Matthijs de Ligt kuwa habari zinazosema ameshamalizana na Paris Saint-Germain hazina ukweli wowote, ni uongo mtupu.

Beki huyo amekuwa gumzo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, akihusishwa na klabu kibao zikiwamo Manchester United na Barcelona.

Lakini Raiola, anayemsimamia pia kiungo wa Man United, Paul Pogba alisema kinachosemwa De Ligt ameshamalizana na PSG hakina ukweli wowote.

De Ligt, 19, amecheza kwa kiwango bora msimu uliopita na kuisaidia Ajax kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanya huduma yake kusakwa kila kona. Ajax inamthaminisha beki wake huyo kuwa na thamani ya Pauni 60 milioni.

Mapema wiki hii kulikuwa na taarifa kwamba PSG imeweka mambo sawa kwenye kumnasa staa huyo huku ikiripotiwa itamlipa mshahara wa Pauni 211,000 kwa wiki.

Huko nyuma ilielezwa pia De Ligt alikuwa anakaribia kutua Barcelona kabla ya habari kama hizo kuwahusu Man United na mahasimu wao Manchester City. Lakini Raiola alisema kuhusu PSG, “Habari za uongo.

“Mnasema picha yangu na mwandishi wa habari wa Kifaransa niliyopiga Paris? Yeye alikuja kuniomba tupige picha, sikumfahamu ni nani. Sijawahi kuzungumza naye.”

De Ligt alisema mwenyewe pesa haiwezi kuamua hatima yake ya klabu gani atakwenda, akisema: “Pesa sio tatizo. Kitu muhimu ni kufahamu timu gani unakwenda ambayo itakupa umuhimu na nafasi ya kucheza mechi nyingi. Sijui bado nitakwenda wapi, kwa sasa nipo likizo, nitaamua wapi pa kwenda.”