Raila: Msiwaogope Everton FC, wanafungika hawa!

Muktasari:

Hii ni mara ya pili, kwa timu hizi kukutana , kwani mara ya kwanza, Ilikuwa mwaka jana katika Uwanja wa Taifa, Dare es Salaam, na Toffees wakaibuka washindi wa 2-1, wafungaji wakiwa ni Wayne Rooney na Kieran Dowell, huku bao la Kogalo likiwekwa kimiani Jacques Tuyisenge.

Nairobi, Kenya. Mlezi wa timu ya Gor Mahia, Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Amollo Odinga, ambaye yupo nchini England, kuipa sapoti timu, itakapowakabili Everton katika mechi ya kirafiki baadae leo, amewataka wachezaji wa Kogalo, kutokuwa na hofu, kwani Everrton, Wanafungika tu.
Akizungumza na wachezaji hao, alipowatembelea katika hoteli waliofikia, Jijini Liverpool, Raila aliwataka Gor Mahia kutokuwa na hofu ya aina yoyote kuelekea mechi hiyo, itakayopigwa ugani Goodison Park, kuanzia saa 4:00 usiku, kwani Afrika Mashariki na Afrika iko nyuma yao.
Raia ambaye ameandamana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo, Kirimi Kaberia, Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambroce Rachier na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya SporPesa, Captain Ronald Karauri, amewataka Kogalo kujiamini na kucheza mchezo wao.
“Ingieni uwanjani na kucheza mchezo wenu bila hofu, hao Everton ni wanaume kama nyinyi, wana mbili na nyinyi mna mbili, msihofu kwa sababu tuko nyuma yenu, Afrika yote iko nyuma, Afrika Mashariki inawaombea, Kenya inawategemea,” alisema Raila.
Mabingwa hao mara 17 wa KPL, walipata fursa ya kukutana na Everton kwa mara ya pili, baada ya kuifunga Simba FC ya Tanzania 2-0, mapema mwaka huu, katika mechi ya fainali ya kombe la SportPesa, iliyopigwa ugani Afraha Nakuru.
Mara ya kwanza kukutana na Everton FC, Ilikuwa mwaka jana katika uwanja wa Taifa, Dare Es Salaam, ambapo Everton FC, ambao walifanya safari yao ya kwanza kuja Afrika, walishinda 2-1, mabao yakifungwa na Wayne Rooney na Kieran Dowell. Bao la Kogalo lilifungwa na Jacques Tuyisenge.