Rage mikononi mwa Takukuru, aachiwa

Muktasari:

Rage aliiongoza Simba akiwa mwenyekiti kuanzia mwaka 2010 hadi 2014 na kabla ya hapo aliwahi kuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT).

Miaka 12 baada ya kushinda rufaa ya matumizi mabaya ya ofisi ndani ya kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amejikuta akitua mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tabora akituhumiwa kujihusisha na matendo yanayoashiria rushwa.

Mkuu wa Takukuru mkoani Tabora, Mussa Chaulo alisema kuwa taasisi hiyo ilimshikilia Rage kuanzia Jumamosi hadi Jumapili ya wiki iliyopita ilipomuachia kwa dhamana.

"Mnamo tarehe 23 Mei 2020, TAKUKURU mkoa wa Tabora ilimshikilia Bwana Ismail Aden Rage, Mkurugenzi wa Voice of Tabora FM Redio kwa tuhuma za rushwa na kuanza kampeni kabla ya wakati.

 Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya taarifa kutoka chanzo cha siri ikieleza kuwa katika maeneo kadhaa ndani ya Manispaa ya Tabora kwa nyakati tofauti alikusanya wapiga kura ambao ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Kata na Matawi kwa lengo la kuwashawishi wampigie kura.

Ili kutoharibu uchunguzi unaoendelea Bw. Ismail Aden Rage alilazwa mahabusu kuanzia tarehe 23 Mei 2020 hadi tarehe 24 Mei 2020 alipoachiwa kwa dhamana. Uchunguzi wa taarifa hii unaendelea mara utakapokamilika taarifa kamili itatolewa kupitia vyombo vya habari," alisema Chaulo katika  taarifa yake aliyoitoa leo.

Akizungumza na Mwanaspoti Online Rage alikiri kuhojiwa na mamlaka hiyo inayojihusisha na udhibiti wa rushwa nchini.

"Nimepigiwa simu na watu zaidi ya 200 wakiniuliza kuwa bado nipo mahabusu lakini ingekuwa hivyo tusingekuwa tunazungumza hapa.

Kiufupi kipindi kama hiki mambo hayo yanatokea na mimi ni kweli waliniita tu kunihoji na baada ya hapo wakaniachia nipo naendelea na shughuli zangu," alisema Rage.

Mwaka 2008, Rage alishinda rufaa ya kupinga adhabu ya kifungo cha miaka mitatu (3) aliyopewa mwaka 2005 kwa kosa la kuiba zaidi ya Sh3milioni , ikiwa ni fedha taslimu na vifaa vya TFF wakati huo akiwa katibu mkuu kilipokuwa kikijulikana kama FAT.

Hata hivyo rufaa hiyo ambayo Rage alishinda, ilitolewa uamuzi wakati akiwa huru baada ya kupewa msamaha na Rais Benjamin Mkapa alipokuwa anamaliza muda wake mwaka huohuo 2015.