Rage afichua adhabu za Eymael

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage aliyewahi kuwa kiongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF, tangu enzi za FAT), alisema kilichofanywa na Kocha Eymael hakikubaliki na matusi aliyoyatoa hayawahusu Yanga pekee bali hta wao Simba kama sehemu ya Watanzania na kueleza kama TFF itaitengeneza kesi ya Mbelgiji huyo vizuri Fifa kuna uwezekano mkubwa wa kufutiwa leseni yake ya ukocha, kupigwa faini ama kupewa kifungo cha muda kutegemeana na kesi itakavyomkalia.

“Fifa imekuwa ikipinga na kulaani ubaguzi wa aina yoyote na wamekuwa wakali mno, kama TFF itampeleka Fifa na ikaitengeneza kesi hiyo kwa namna itakavyojiridhisha na kauli zake za kibaguzi, Kocha Eymael anaweza kupoteza leseni yake, kufungiwa sambamba na kulimwa faini kali,” alisema Rage na kuongeza;

“Kwa kweli alichokifanya huyu kocha ni udhalilishaji wa Watanzania, nalisema hili kwa dhati na kuwataka wanasimba wasicheke na kuwatania wenzao, kwani tusi hili ni la Watanzania wote na kocha wa aina hii hatufai hata kidogo,” alisema Rage.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 41 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, adhabu ya kosa kama lililofanywa na Eymael huwa ni faini ya fedha na kifungo.

“Kocha yeyote atakayebainika/kuthibitika kushiriki/kufanya kitendo chochote kingine cha uvunjaji taratibu au ukiukaji mwingine wowote taratibu kwa mujibu wa kanuni hizi au taratibu nyingine za uendeshaji Ligi Kuu ambao haukuainishwa katika kanuni hii ataadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali au Karipio na/au faini kati ya Sh. 300,000 (laki tatu) mpaka Sh3 milioni, na/au kufungiwa kwa kipindi kati ya miezi mitatu mpaka miezi ishirini na nne au michezo kati ya mitatu mpaka kumi.