Rabiot amtilia kauzibe Ramsey kutua Juventus

Muktasari:

  • Baada ya mazungumzo ya kuongeza mkataba baina ya Aaron Ramsey na Arsenal kuvunjika, kiungo huyo ana uwezekano mkubwa wa kujiunga na mabingwa wa Italia, Juventus ambayo wamemuweka namba mbili kati ya viungo inaowahitaji, itampa nafasi ya kwanza iwapo itamkosa Adrien Rabiot wa PSG anayefukuziwa pia na Barcelona.

 

Milan, Italia. Kama kuna mtu anayemzibia riziki Aaron Ramsey wa Arsenal kutua Juventus, basi atakuwa kiungo wa PSG, Adrien Rabiot.

Ramsey ameshafunguliwa mlango Emirates na timu ambayo inamnyemelea ni Juventus, lakini nayo inasubiri kwanza ijiridhishe kwamba imemkosa Rabiot ndipo imgeukie yeye.

Arsenal imekataa kumpa Ramsey mkataba mpya jambo linaloashiria yupo huru kuanza mazungumzo na timu yoyote kwa kuwa mkataba wake wa sasa utamalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Ramsey anaweza kusajiliwa na Juventus iwapo klabu hiyo itamkosa kiungo wa Ufaransa Rabiot,”umesema mtandao mmoja mapema leo.

Kwa upande wake Raboit amezitema ofa nne za kutaka kuongeza mkataba kutoka PSG, kwa kinachoelezwa anavizia ofa nono kutoka Barcelona, Liverpool na Juventus.

Pamoja na hayo imebainika kuwa Ramsey naye anawindwa pia na AC Milan, Chelsea, Manchester United na Liverpool.

Mazungumzo baina ya Arsenal na Ramsey yalivunjika baada ya kutaka aongezewe mshahara kutoka huu wa sasa anaolipwa Pauni 110,000 kwa wiki, kufikia Pauni 300,000 kwa wiki sawa na anaolipwa Mesut Ozil lakini kocha wake, Unai Emery akakataa.

Ramsey alijiunga na Arsenal mwaka 2008 na ameshaitumikia katika mechi 242 na kufunga mabao 37 katika michuano mbali mbali.