RVP abamba dili la kuchambua soka

Muktasari:

Mdachi huyo alifunga mabao 26 katika msimu wake wa kwanza Old Trafford na kubeba taji la Ligi Kuu England. Kwa miaka yake mitatu aliyodumu na Man United, Van Persie alicheza mechi 105 na kufunga mabao 58 na kuondoka kutimkia huko Uturuki, alikojiunga na Fenerbahce.

LONDON, ENGLAND.STRAIKA matata Robin van Persie ameripotiwa kwamba atakwenda kujiunga na BT Sport kwa ajili ya kufanya kazi ya uchambuzi kuanzia msimu ujao.
Gwiji huyo wa Manchester United na Arsenal sasa ataungana na wakali wengine wa zamani kama Rio Ferdinand na Martin Keown kwenye studio wakifanya uchambuzi wa mechi mbalimbali za Ligi Kuu England na nyinginezo baada ya kutangaza kustaafu soka Mei mwaka huu.
Van Persie amefurahia kucheza soka la kiwango cha juu sana, akianzia huko Excelsior kabla ya kwenda kujiunga na Feyenoord.
Alishinda ubingwa wa Kombe la UEFA mwaka 2002  kabla ya kunaswa na Arsenal miaka miwili baadaye.
Straika huyo aliyefahamika kwa kifupi kama RVP, alifunga mabao 132 katika mechi 278 alizochezea Arsenal chini ya kocha Arsene Wenger, lakini alifanikiwa kushinda taji moja tu la Kombe la FA kwa miaka yote nane aliyokuwa kwenye kikosi hicho kabla ya kunaswa na Man United ya kocha Sir Alex Ferguson mwaka 2012.
Mdachi huyo alifunga mabao 26 katika msimu wake wa kwanza Old Trafford na kubeba taji la Ligi Kuu England. Kwa miaka yake mitatu aliyodumu na Man United, Van Persie alicheza mechi 105 na kufunga mabao 58 na kuondoka kutimkia huko Uturuki, alikojiunga na Fenerbahce.
Van Persie alirudi zake Feyenoord na kushinda Kombe la Uhoanzi mwaka 2018 na kubaki hapo hadi alipoamua kuyapa kisogo maisha ya soka kama mchezaji. Katika kikosi cha timu ya taifaya Uholanzi, RVP amefunga mabao 50 katika mechi 102 na kuisaidia timu hiyo kushinda namba mbili kwenye Kombe la Dunia 2010 na namba tatu kwenye Kombe la Dunia 2014. Lakini, sasa msimu ujao mashabiki watamwona nyuma ya televisheni zao akifanya kazi ya uchambuzi wa mechi.