Programu Stars yaacha kilio Simba, Yanga

Muktasari:

Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kuondoka leo usiku kwenda Cape Verde kucheza mchezo wa kufuzu fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani Cameroon.

Hata hivyo, Taifa Stars itaondoka na wachezaji watatu wa timu za Simba na Yanga waliopata majeraha wakati wakizitumikia klabu zao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Programu ya timu ya Taifa 'Taifa Stars' imeanza kuleta kilio kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zikihofia kuumia au kushuka ufanisi kwa nyota wao muhimu walioitwa kukitumikia kikosi hicho.

Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kufuzu Fainali za Afrika mwakani zitakazofanyika Cameroon, ilianza kambi Oktoba Mosi jijini kujiandaa na mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Cape Verde zitakazochezwa Oktoba 12 na 16.

Kutokana na ugumu na umuhimu wa mechi hizo mbili, benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Emmanuel Amunike, liliomba wachezaji walioitwa katika kikosi hicho kutoka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kuingia kambini mapema kupata maandalizi mazuri ya kiufundi kabla ya kuivaa  Cape Verde.

Hata hivyo, Bodi ya Ligi ilitangaza uamuzi wa kuendelea na mechi za Ligi Kuu kama zilivyopangwa wakati kambi ya Taifa Stars ikiendelea.

Badala ya kuahirisha baadhi  ya mechi za Ligi Kuu ili kutoa fursa kwa benchi la ufundi la Taifa Stars kupata muda wa kutosha wa maandalizi, bodi iliamua mechi za ligi kuendelea kuchezwa kama kawaida huku wachezaji wa timu ya Taifa wakiwekewa utaratibu wa kwenda kuzitumikia timu zao katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki na kurejea kwenye kambi ya Taifa Stars.

Uamuzi huo ulifanyika siku chache baada ya bodi hiyo kusogeza mbele mechi ya Simba dhidi ya Biashara United na Yanga na JKT Tanzania kwa lengo la kuzipa nafasi kujiandaa na mechi ya watani wa jadi baina yao iliyochezwa Septemba 30.

Hatua hiyo imezilazimisha klabu husika kufanya programu za maandalizi ya mechi zilizocheza mwishoni mwa wiki iliyopita bila uwepo wa nyota wa Taifa Stars ingawa zilipata nafasi ya kuwatumia katika mechi hizo jambo ambalo lina madhara kiufundi.

Wakati uamuzi wa kuwarudisha wachezaji kutumika kwenye timu zao na kurejea timu ya Taifa, umeibua hofu ya majeruhi jambo ambalo nusura lizigharimu baadhi ya klabu hasa Simba na Yanga ambazo zilicheza Jumamosi na Jumapili dhidi ya timu za African Lyon na Mbao.

Katika mchezo dhidi ya African Lyon, nyota wawili wa Simba, Jonas Mkude na Shomari Kapombe walipata majeraha na siku moja baadaye Andrew Vincent 'Dante' na kipa Beno Kakolanya wa Yanga walishindwa kumaliza mechi dhidi ya Mbao, baada ya kupata majeraha sanjari na Kelvin Yondani ingawa alimaliza mechi hiyo.

Wachezaji wote watano walipata majeraha yanayofanana ambayo ni kubanwa na misuli, tatizo ambalo mara kwa mara linachangiwa na wachezaji kufanya mazoezi magumu.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema ameshangazwa na kitendo cha wachezaji kufanyishwa programu za mazoezi mara mbili kwa siku.

"Simba inaweza kufanya vizuri bila uwepo wa hao wachezaji ambao wamekwenda kwenye kambi ya timu ya Taifa, lakini wasiwasi wangu ni programu ambazo wamekuwa wakifanya  zinaweza kuchangia kuwaumiza au wakashindwa kuonyesha ufanisi.

Kwa kawaida mchezaji anapokuwa kwenye timu ya Taifa hapaswi kufanyishwa mazoezi magumu, lakini nashangaa kuona wachezaji hapa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni jambo ambalo lina athari kwa wachezaji lakini kwa timu na kipindi kama hiki hakuna kocha anayeweza kukubali kuwakosa wachezaji," alisema Aussems.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema kuwa aina ya majeraha ambayo wachezaji wake wamepata dhidi ya Mbao yana uhusiano wa moja kwa moja na aina ya programu wanazopata timu ya Taifa.

"Sipendi kuzungumzia programu za timu ya Taifa, lakini ukiangalia wachezaji wangu Dante na Kakolanya wote kwa pamoja wamepata majeraha ya kubanwa na misuli, hivyo unaweza kuona au kuhisi wanafanyishwa mazoezi magumu.

Nadhani kunatakiwa kuwepo na programu zitakazowaepusha wachezaji kutopata majeraha," alisema Mwandila.