Prisons yatumia Dk 1,260 kinyonge

Muktasari:

  • Katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa Prisons imeshinda mechi mbili, ikitoka sare 9 na kupoteza mechi 9.

HATA wenyewe hawaamini, lakini ukweli ni kwamba Tanzania Prisons imetumia dakika 1,260 ili kufuta unyonge katika Ligi Kuu kwa kupata ushindi wa pili tangu msimu huu uanze Agosti 22, mwaka jana.

Prisons waliiotea Mtibwa Sugar juzi kwa kuwanyuka mabao 2-0 ukiwa ni ushindi wao wa kwanza tangu waliposhinda mara ya kwanza na mwisho Septemba Mosi, mwaka jana walipoizabua Alliance kwa mabao 2-0.

Ndani ya dakika hizo 1260, Prisons ilikuwa haijawahi kupata ushindi zaidi ya sare ama kuambulia vipigo na kuwafanya wakusanye alama 13 tu kabla ya ya ushindi wa juzi kuwafanya wafikishe alama 15 na kutoka mkiani hadi nafasi ya 19.

Katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa Prisons imeshinda mechi mbili, ikitoka sare 9 na kupoteza mechi 9.

Akizungumza na Mwanaspoti, nahodha wa Prisons, Laulian Mpalile alimshukuru Mungu kwa kupata matokeo hayo ambayo yaliyowaondolea unyonge wa muda mrefu, ambapo hawakuwahi kukutana nayo.

Alisema ushindi huo wanautumia kama chachu ya mafanikio ni mabadiliko ya benchi la ufundi.

“Mwalimu kaanza kutuongoza katika mchezo wetu dhidi ya Lipuli tulifungwa, lakini hakukata tamaa alikaa nasi na kutuambia tunakosea wapi na kwa siku tano kabla ya kuvaana na Mtibwa Sugar alitumia kutujenga vyema na tumepata matokeo,” alisema.

Mpalile alisema hawajakata tamaa na wala Prisons haitashuka daraja kwani, bado wanamichezo 18 mbele yao ambayo kama wataitumia vizuri itawanusuru na janga hilo.

Kwa sasa Tanzania Prisons iko mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikipambana kusaka ushindi ili kujinasua kwenye wimbi la kushuka daraja, ambapo kwa kauli ya Mpalile ni kuwa, watapambana sana.