Prince Dube anakupiga kotekote

NDANI ya muda mfupi straika mpya wa Azam FC, Prince Dube amejitengenezea ufalme klabuni hapo, huku akiwakuna mashabiki wengi wa soka nchini kwa umahiri wa kucheka na nyavu.

Dube aliyesajiliwa na Azam msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Highlanders FC ya Zimbabwe, tangu aanze kukinukisha katika Ligi Kuu Bara amethibitisha Wanalambalamba hawajapoteza fedha zao kumnasa.

Kupitia mechi tano za Ligi Kuu na nyingine alizoitumikia Azam hadi sasa ameonyesha ni straika wa aina gani ambaye klabu hiyo ilikuwa ikimsaka tangu ilipoondokewa na Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast. Mkali huyo katika mechi tano za Ligi Kuu amefunga mabao matano ikiwa ni wastani wa kila mechi bao moja na pia ameasisti mara mbili mbali na mechi za kirafiki alizocheza na kuonyesha uwezo mkubwa.

Mwanaspoti linakuletea japo kwa ufupi namna Dube alivyojitengenezea ufalme mapema katika Ligi Kuu Bara, kwani jamaa kokote anakupiga kama timu pinzani zinamkalia vibaya kwenye ligi iliyosimama kwa muda kupisha mechi za kirafiki za kimataifa.

BAO LA KIRAFIKI

Dube alianza kuonyesha makeke kwenye utupiaji mara baada ya kuichezea kwa mara ya kwanza Azam katika mchezo wa kirafiki ambapo alifunga bao pekee lililowazima KMC.

Katika mchezo huo alifunga bao hilo sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho akipokea pasi kutoka kwa Obrey Chirwa na akiwa ndani ya 18 alitumia akili na utulivu kutumbukiza mpira wavuni na kuanza kufungua akaunti yake ya mabao.

MECHI TATU BAO TANO

Unaweza kushangaa, lakini ukweli ni kwamba Dube ni aina ya washambuliaji halisi ambaye anajua kuifanya kazi yake kwa kufunga kila anapopata nafasi mbele ya lango la timu pinzani.

Dube ameonyesha uzuri wake kwani katika mechi tano ambazo amecheza ametoa pasi za mabao mawili katika Ligi Kuu, huku akitumia michezo mitatu tu kufunga mabao matano yaliyomuweka kileleni kwenye orodha ya wafungaji.

Straika huyo alianza kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union, kisha akafunga bao pekee dhidi ya Tanzania Prisons walipoichapa 1-0 na kumalizia kwenye mchezo waliopata ushindi mnono wa mabao 4-2 dhidi ya Kagera Sugar.

KWA KICHWA HATARI

Jamaa amekamilika kwani kwani anapokuwa ndani ya 18 anaweza kufunga kwa staili yoyote ile ilimradi tu mpira uende wavuni.

Katika mabao matano aliyofunga, katupia bao moja kwa kichwa kuonyesha sio mtu wa mchezomchezo. Bao hilo alilifunga dhidi ya Prisons dakika 90 akiunganisha krosi ya Idd Seleman ‘Nado’.

MIGUUNI NDIO BALAA

Achana na kutupia kwa kichwa, kwenye miguu jamaa ndio balaa zaidi kwani hachagui wa kutupia mpira kambani, iwe kulia ama kushoto freshi tu!

Katika mabao matano, ukiondoa la kichwa, manne yaliyobaki kila mguu amefunga mawili, yaani mawili kulia na mengine kushoto kuthibitisha anapokuwa kazini hachagui silaha ya kutumia.

Dube alionyesha ni balaa kwa kutumia miguu miwili wakati akiiadhibu Coastal Union kwa kufunga mabao ya kwanza katika Ligi Kuu, msimu huu.

Alianza kwa kufunga kwa mguu wa kushoto akimalizia pasi murua ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kabla ya kufunga la pili kwa mguu wa kulia akimalizia pasi ndefu ya Oscar Masai aliyokutana nayo ndani ya boksi na kufanya yake.

Kama unadhani alibahatisha kwa Wagosi utakosea, kwani jamaa alirudia tena kitendo hicho kuzitungua timu pinzani kwa miguu yote walipomalizana na Kagera Sugar na kuwafumua mabao 4-2.

Mzimbabwe huyo alifunga mabao mawili - la kwanza likitokana na pasi ndefu ya ndani ya boksi kutoka kwa Obrey Chirwa akaunganisha wavuni kwa mguu wa kulia kisha kuongeza jingine la pili kwa guu la kushoto akiunganisha krosi Idd Seleman ‘Nado’.

ISHU NJE YA BOKSI

Licha ya Dube kuonekana mchezaji hatari akiwa ndani ya 18, lakini ana kazi ya kuwathibitishia mashabiki kwamba hata nje ya eneo hilo ni balaa, kwani mpaka sasa hajaonyesha makali.

Dube anaonekana ni mtamu akiwa ndani ya 18 na ana kibarua cha kuonyesha ni moto nje ya eneo hilo na hilo ataweza kulithibitisha kwenye michezo 12 ya duru la kwanza na 17 ya duru la pili, ili kukamilisha mechi 34 za timu yake katika msimu wake wa kwanza Azam FC.

Hata hivyo, kwa kasi aliyoanza nayo ni wazi inawapa kibarua kizito mabeki wa timu pinzani ambao sasa watatakiwa watambue kuwa Dube sio mtu mzuri anapokuwa ndani ya boksi kwani kumruhusu apokee mpira ndani ya eneo hilo, basi wajue atawaliza mapema.

KWA PASI NI NOMA

Mabeki hawapaswi tu kumchunga Dube asiwatie aibu langoni kwao, lakini pia wana kibarua cha kuhakikisha hata zile pasi zake matata hazipigi na hapati nafasi ya kuwatengenezea wenzake mabao.

Katika mechi tano za ligi, Dube ametengeneza mabao mawili akitoa pasi murua kwa Chirwa ambaye hakuwa na hiyana zaidi ya kuzikwamisha wavuni na kuwa mabao yake pekee mpaka sasa.

Alimtengenezea pasi ya bao katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania na kwenye pambano la Kagera Sugar.

Mwenyewe aliwahi kusema kazi yake ni kufunga na huwa na furaha anapofunga na hasa kuisaidia timu kupata matokeo mazuri, kwani ndio kazi ya mshambuliaji.

Kocha Mkuu wake, Aristica Cioaba aliliambia Mwanaspoti mwanzoni mwa msimu kwamba hawezi kumzungumza Dube akitaka kwanza acheze mechi sita ili kuona kama ataendeleza moto ule ule na sasa kamthibitishia.