Poulsen bado hajapoa huko Bundesliga

Muktasari:

 Poulsen ni Mdenmark mwenye asili ya Tanzania ameanza na moto wa aina yake kwenye msimu wa 2018/19 kwa kufunga mabao manne kwenye michezo saba ya Bundesliga

 

HUU unaweza kuwa miongoni mwa misimu bora kwa mshambuliaji mwenye asili ya Tanzania, Yussuf Yurary Poulsen anayeichezea RB Leipzig ya Bendesliga, Ujerumani.

Poulsen ambaye asili yake ni Tanga, Tanzania ameanza na moto wa aina yake kwenye msimu wa 2018/19 kwa kufunga mabao manne kwenye michezo saba ya Bundesliga.

Kuna kila dalili kwa nyota huyo kuendelea kufanya vizuri kutokana na maelewano mazuri na Werner Timo ambaye amekuwa akicheza naye kwenye safu ya ushambuliaji ya Leipzig.

Ndani ya michezo saba, Poulsen amefikia idadi ya mabao aliyoyafunga msimu uliopita wa 2017/18 ambapo alifunga mabao manne kwenye Bundesliga katika michezo 30.

Idadi kubwa zaidi ya mabao kwa Poulsen kufunga ndani ya msimu mmoja wa Bundesliga kwa mshambuliaji huyo ilikuwa msimu wa 2014/15 ambao alifunga mabao 11.