Porto, Celtic zaanga Ligi ya Mabingwa, Ajax chupuchupu

Wednesday August 14 2019

 

London, England. Porto na Celtic zimeanga mapema mashindano ya Ligi ya mabingwa huku Ajax ikiponea tundu la sindano kufuzu kwa hatua ya mwisho ya kucheza hatua ya makundi ya mashindano hayo,

Mabingwa 2004, Porto wanashinda kufuzu kwa mara ya kwanza kwa hatua ya makundi tangu msimu 2010-11, wakati Celtic ikirudia rekodi yake mbaya ya msimu uliopita.

Mabingwa hao wa Ureno, Porto ilishinda mchezo wa kwanza bao 1-0, lakini katika mchezo wa marudiano walikubali kuruhusu mabao 3-0 kutoka kwa FC Krasnodar ya Russia kwenye Uwanja do Dragao.

Porto iliamka kipindi cha pili na kupata mabao mawili yaliyofungwa na Ze Luis na Luis Diaz, lakini mwisho mchezo wakafungwa 3-2 kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 na Wareno hao kuondolewa kwa sheria ya bao ya ugenini.

Nayo Celtic ilipoteza nafasi ya kusonga mbele kwa mashindano hayo baada ya kuondolewa na CFR Cluj jijini Glasgow.

Mabingwa hao wa Scotland walifungwa 4-3 na kuondolewa kwa matokeo ya jumla ya mabao 5-4 na timu hiyo ya Romania.

Advertisement

Celtic kuondolewa katika hatua hii ni mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kutolewa na AEK Athens katika hatua hiyo.

Pamoja na kucheza nusu fainali msimu uliopita Ajax ililazimika kutoka nyuma kwa bao moja kabla ya kuwafunga mabingwa wa Ugiriki, PAOK 3-2 nyumbani na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4.

Mabingwa wa zamani Red Star Belgrade imeitoa FC Copenhagen kwa penalti 7-6, huku ikishuhudiwa penalti tisa (9) zikiota mbawa kati ya penalti 22 zilizopigwa.

Mechi hiyo ilimalizika kwa sare 1-1 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 nchini Denmark ndipo penalti zilipotumika kupata mshindi.

Club Bruges nayo imefuzu kwa mbinde baada ya kulazimishwa sare 3-3 na Dynamo Kiev ya Ukraine, lakini wameshinda kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Mechi hiyo ilishuhudia timu hizo zikipoteza wachezaji kwa kadi nyekundu katika muda wa majeruhi na timu zote zikifunga mabao katika dakika za majeruhi.

Advertisement