Pongezi zamiminika Bandari kufuzu Kombe la Shirikisho

Muktasari:

Ramos Mwashigadi wa Wundanyi anasema Bandari inaweza kufika mbali sana kwenye mashindano hayo kutokana na wachezaji wake kupata uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

MOMBASA. RISALA zinazidi kufurika katika ofisi za Mwanaspoti, mjini Mombasa za kuipongeza Bandari FC kwa kuilazimisha timu ya Al Ahli Shandy sare ya kufungana bao 1-1 katika mechi iliyochezwa Sudan na kufuzu kwa raundi ya pili ya Caf Confederation Cup.

Hata hivyo, wengi waliotuma jumbe zao wameeleza kuhuzunika kuwa hawashuhudii mechi za timu yao hiyo ikicheza hata mechi za nyumbani za mashindano hayo ya barani Afrika.

Wamelaumu ucheleweshaji wa ujenzi wa Uwanja wa Kaunti ya Mombasa.

Shabiki Abdalla Sadiki wa Kwale anaipongeza Bandari kwa kufanikiwa kufuzu raundi ya pili ya mashindano hayo na akaitakia heri ifanikiwe kusonga mbele zaidi.

“Nina huzuni kuwa hatutaiona timu yetu ikicheza mechi ya nyumbani kwa ukosefu wa uwanja,” akasema.

Ramos Mwashigadi wa Wundanyi anasema Bandari inaweza kufika mbali sana kwenye mashindano hayo kutokana na wachezaji wake kupata uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

“Tunaomba magavana wa Pwani watujengee uwanja tuzione timu zetu,” akasema.

Naye Kocha wa Skyward Express FC ya Lamu, Mohammed Dadi amesema ushindi wa Bandari ni fahari kwa soka la Pwani na akataka wachezaji wazidi kufanya mazoezi ili waweze kufika mbali n ahata kuibuka washindi.

“Tunataka Bandari FC iweke historia mpya ya soka la pwani kwa kuwa timu ya kwanza kubeba kombe hilo la Caf na nina imani kubwa kikosi kilichoko, kinaweza kuwika na kushinda,” akasema.

Mashabiki wengine Abdul Samad wa Malindi, Kenga Karisa wa Mariakani na Hamisi Ali wa Hola wote wametoa pendekezo serikali sita za kaunti za Mkoa wa Pwani zishirikiane kuujenga Uwanja wa Kaunti ya Mombasa kwani wapenzi wa soka mkoani wanakosa uhondo.