Pondamali: African Sport itapanda daraja

Friday July 10 2020

 

By IMANI MAKONGORO

KOCHA Juma Pondamali ameanza kupiga hesabu ya African Sport kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Kocha huyo na kipa zamani wa Yanga amesema ndoto yake ni kuipandisha African Sport hadi Ligi Kuu.

"Tuko mguu ndani mguu nje kufuzu kucheza FDL naamini mechi yetu ya leo Ijumaa itakuwa ni nafasi tosha ya kufikia ndoto zetu," amesema.

African Sport itacheza nusu fainali ya kwanza ya Ligi Daraja la Pili (SDL) leo saa 8 mchana dhidi ya Shule ya Fountain Gate ya Dodoma.

Mechi hiyo itapigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, ikifuatiwa na ile ya Kitayosa ya Tabora dhidi ya Mbuni saa 10 jioni.

Akizungumzia maandalizi yao, Pondamali amesema wako vizuri na kusisitiza kuwa wana matumaini ya ushindi.

"Tumepambana kwa nguvu, juhudi na malengo, dakika 90 za mechi yetu ya leo ndiyo kila kitu kwetu katika kutimiza ndoto yetu ya kupanda daraja," amesema.

Kocha huyo amesema ndoto yake ni kurudi kufundisha Ligi Kuu akiwa na timu ya African Sport miaka ijayo.

"Tunafahamu ugumu wa mechi yetu ya leo, lakini tumejipanga na tunaamini tutafanya vizuri," amesema.

African Sport inashiriki mechi za nusu fainali ambayo itawawezesha kutinga fainali na kupatikana mshinda atakayepanda FDL.

Advertisement