Pollack aipa tano Gor Mahia kusonga mbele CAF

Tuesday August 27 2019

 

By Thomas matiko

KOCHA mpya wa Gor Mahia, Mwingereza Steven Pollack kasifia ushindi mkubwa waliousajili Jumapili uwanjani Kasarani dhidi ya Waburundi Aigle Noir wa mabao 5-1, mchezo wa marudio kuwania kufuzu hatua ya makundi ya dimba la CAF Champions League.

Wakicheza nyumbani baada ya kutoka sare tasa ugenini jijini Bunjumbura, wageni hao walikosa ujanja mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu huku straika Nicholas Kipkurui akiwa mwiba hatari kwenye ngome ya difensi yao.

Kwenye mchezo huo, Kipkurui alipachika mabao matatu, huku moja lilikataliwa, pia kutoa asisti ya bao lingine.

Baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, Gor walikuwa tayari wameshazalisha matoke makubwa kinyume na walichohitaji. Gor walihitaji ushindi wa angalau bao moja ili kusonga mbele kwa faida ya mabao lakini wakaishia kuwatia aibu Noir.

Akifunguka baada ya mchuano Pollack alisema, kilichosaidia timu yake zaidi ni mazoezi mazuri ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa wiki nzima. “Hakika nimefurahishwa na matokeo. Kulikuwa na ishu ya safu ya mbele kuwa butu ila ni kitu ambacho nimegundua ni cha kawaida Afrika. Timu nyingi hazina mafowadi wenye levo ya juu ya umakinifu na ndio maana nikajifunza kuja na mbinu za kuwasaidia kwa kuhakikisha wanasaidiana kama timu kusaka mabao badala ya kumtegemea mtu mmoja.. Hakika ushindi huu ni mazao ya aina ya mazoezi ambayo tumekuwa tukifanya,” Pollack kafafanua.

Sasa Gor watachuana na USM Algeirs kwenye raundi ya pili ya mchujo, mechi ya kwanza ikichezwa ugenini kule Algers kati ya Septemba 13-15. Baadaye zitarudiana Nairobi huku mshindi akijikatia tiketi ya kuingia kwenye hatua ya makundi.

Advertisement

Advertisement